Habari za Punde

Washindi wa tuzo za umahiri wa uandishi wa habari wa takwimu za wanawake na uongozi kujulikana 25 Febuari, 2023

 


Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ), kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Jumuiya ya Mazingira, Jinsia na Utetezi Pemba (PEGAO) Jumamosi tarehe 25 Febuari, 2023 zimeandaa hafla ya utoaji tuzo maalum za umahiri wa uandishi wa habari za takwimu zinazohusu masuala ya wanawake na uongozi Zanzibar ambayo itafanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil

Kikwajuni kuanzia saa 1: 00 usiku.

 

Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi katika hafla hiyo ambayo inategemewa kuhusisha zaidi ya watu 150.

 

Kauli mbiu ya tunzo hizo ni “KALAMU YANGU MCHANGO WANGU KWA WANAWAKE” na ina lengo la kuimarisha kada ya habari katika eneo mahsusi la takwimu za wanawake hivyo kuwashajiisha waandishi wa habari kutumia kalamu zao katika kuandika kwa weledi na umahiri masuala ya wanawake na uongozi.

 

Waandishi wa habari ni watu muhimu katika kuleta mabadiliko, hivyo wana nafasi kubwa ya kushajihisha kufikiwa kwa usawa wa kijinsia katika vyombo vya maamuzi ikiwa wataandika habari za takwimu na uchambuzi mfululizo.

 

Kazi zilizopitiwa zilikuwa ni 421 kutoka vyombo vya habari vya aina zote vikiwemo magazeti, redio, televisheni pamoja mitandao ya kijamii.


Kazi zilizowasilishwa zilitakiwa ziwe zimetolewa au kurushwa hewani kuanzia Januari 2022 hadi Disemba 31, 2022 na ziwe zimezingatia umahiri wa uandishi na uandaaji bora wa vipindi na makala ikiwemo ubunifu, vyanzo vingi na tofauti vya habari, zenye kuweza kuleta mabadiliko, kutoa suluhisho pamoja na kupanga kwa umakini takwimu za wanawake na uongozi.

 

Jumla ya washindi 12 wanatarajiwa kutunukiwa zawadi katika usiku huo maalum; mshindi wa kwanza, wa pili na wa tatu baada ya kupitiwa na jopo la majaji watano wataalamu wa masuala mbali mbali yakiwemo, habari za magazeti, kielektroniki, mitandao ya kijamii, masuala ya wanawake na sheria.

 

Shughuli hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbali mbali kutoka katika taasisi za Serikali, habari, vyuo vikuu, vyama vya siasa, asasi za kiraia na wadau wa masuala ya wanawake.

 

Kazi za washindi zitatangazwa na kuoneshwa kwa lengo la kuwahamasisha waandishi na wadau wa habari kujifunza na kutafuta njia za kuimarisha kazi za wanwake na uongozi.

 

Hii ni mara ya pili kufanyika kwa tuzo hizo za takwimu za wanawake na uongozi chini ya mradi wa Kuinua Wanawawake katika Uongozi (SWIL) Zanziba kwa mashirikiano na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania.

 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.