Habari za Punde

Mhe Hemed ajumuika na waumini wa wa Msikiti wa Ijumaa wa Shangani Mkokotoni katika Sala ya Ijumaa


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdalla akiwasalimia waumini Msikiti wa Ijumaa wa Shangani Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Ibada ya Sala ya Ijumaa

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amejumuika na waumini wa Msikiti wa Ijumaa wa Shangani Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.

 Akiwasalimia waumini wa msikiti huo  baada ya kukamilika kwa Ibada ya swala hio Alhajj Hemed amewataka wazazi na walezi kuendelea kuwalea watoto wao kwa kuzingatia misingi ya dini ya kiislamu, mila na tamaduni za kizanzibari ili kupata kizazi chenye maadili mema.

Alhajj Hemed ameeleza kufurahishwa kwake na namna vijana wa Mkoa huo wanavyoendelea kushikamana na  Dini kama Uislamu ulivyoeleza.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewasisitiza vijana hao kuongeza Bidii kwa kujiendeleza katika fani mbali mbali ili kupata taalama itakayosaidia kuiendeleza jamii yao na taifa kwa ujumla.

Pamoja na hayo Mhe. Hemed amewataka waumini hao kuendelea kudumisha Amani na utulivu uliopo nchini pamoja na kuwa na mashirikiano katika jamii zao.

Alhajji Hemed amesema ni wajibu wa kila mwananchi kuilinda Amani iliyopo nchini hatua ambayo itasaidia kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na  Serikali ya awamu ya Nane  inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt Hussein Ali Mwinyi Katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.

Aidha Alhajj Hemed amesisitiza waumini kuitumia Misikiti kwa kufanya shura zitakazo jadili mambo mbali mbali yanayotokea katika jamii yao.

Akitoa Khutba katika Ibada hiyo Sheikh Muhammad Alhady Alhatimy kutoka Mombasa Kenya amewakumbusha waumini hao kusameheana hasa kipindi hichi cha kuelekea mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Amesema miongoni mwa sifa ya waumini wa kweli ni kusamehe na kuunga udugu ambapo yeyote atakae kwenda  kinyume na hayo ni kukiuka maelekezo aliyokuja nayo Mtume Muhammad (S.A.W).

Aidha Alhajj Hemed amezuru makaburi ya wanazuoni waliozikwa kijijini hapo na kuwaombea Dua.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.