SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema, haitowafumbia macho
watumishi wa umma wasiotaka kuwajibika hasa wanapopelekewa kero za wananchi
kuzitatua kwenye taasisi zao na kutozifanyia kazi kwa wakati sahihi.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein
Ali Mwinyi ameyasema hayo hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege Zanzibar,
kwenye maadhimisho ya miaka miwili ya mfumo wa Sema Na Rais Mwinyi, (SNR).
Alisema mfumo wa SNR umeleta tija kipindi kifupi tokea kuanzishwa
kwak, umepokea malalamiko mengi ya wananchi na asilimia kubwa yamepatiwa
ufumbuzi kwa watu wengi kupatiwa haki zao na kueleza kwamba Serikali
itajitahidi kuondosha kero zaidi za wananchi.
Dk. Mwinyi alitoa onyo kwa baadhi ya watendaji wa taasisi za
Serikali wasiotaka kutatua changamoto za wananchi zinazowasilishwa kwenye
taasisi zao na kuwaeleza kwamba Serikali itawachukulia hatua.
Pia, Rais Dk. Mwinyi aliwaonya baadhi ya watendaji wa taasisi za
Serikali wanaowapa vitisho maofisa wao wanaotoa taarifa za ubadhirifu kwenye
mfumo wa SNR nakuwaahidi kuwapa ulinzi maofisa wanaotishiwa amani na kuwaeleza wafanye
kazi bila woga.
“Asitokee kiongozi yeyeote
wa Serikali, kuwatisha watoa taarifa kupitia mfumo wa SNR” alionya Dk. Mwinyi
Aidha, amewaonya baadhi ya maofisa wa mfumo huo kutohoji mamlaka
wanapofikishiwa maagizo na kero za jamii, badala yake watekeleze wajibu wao kwa
kuzitafutia ufumbuzi unaofaa pamoja na kuwataka watendaji wa serikali kuheshimu
na kutii mamlaka za serikali haswa zinapokuja kesi ya utekelezaji wa maagizo ya
Serikali.
“Kama kuna kitu ambacho hakina sababu, wala hatutaki kusikia ni
kutokuwajibika kwa maofisa wa SNR kwamba hawatowajibika, Ofisa yoyote wa SNR
asietaka kuwajibika, msitegemee Ikulu itachukua hatua, wakuu wa taasisi mko
hapa tusije tukalizungumzia tena hapa” Alionya Rais Mwinyi.
Rais Dk. Mwinyi alisema mfumo huo utaendelea kufanyakazi kwa
karibu na wanachi na kueleza kwamba
mfumo huo una utambuzi wa takwimu kubaini viongozi na taasisi zinazoharibu ama
kufanya vizuri hivyo, alieleza
wakati umefika kila mmoja aone umuhimu wa kuwajibika.
Alizungumzia suala la
taarifa za ubadhirifu wa mali za umma Dk. Mwinyi aliahidi kuchukuliwa kwa hatua
dhidi ya kiongozi asiewajibika kwenye majukumu yake.
Rais Dk. Mwinyi pia alisema
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini uhuru wa Mahakama, hivyo kupitia
mfumo wa SNR Serikali itayafikisha malalamiko ya wananchi kupitia Jaji Mkuu ili
yashughulikiwe mahakamani kwa kuondosha kasoro zinazojitokeza.
Aliitaka Wizara ya Fedha na Mipango kutenga bajeti ya kurejesha
fidia kwa wananchi na kueleza sasa Serikali itahakikisha inalipa fidia kwa
wananchi waliopitiwa na miradi ya maendelo kadri ya wakati ukatavyoruhusu.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Ikulu,
Jamal alisema kuanzishwa kwa mfumo wa SNR ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya nane kwa kuwataka viongozi na watendaji wa ndani
ya Serjali wanawajibika kwa vitendo.
Naye, Mkuu wa kitengo cha Sema Na Rais, Haji Makame alisema tokea
kuanzishwa kwa kitengo hicho miaka miwili iliyopita, kimefanikiwa kupokea
changamoto na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa Unguja na Pemba na
kuyapatia ufumbuzi kwa baadhi yao.
Aliwaeleza mfumo umeziunganisha taasisi 65 za Seriakali na kueleza
kwamba una mpango wa kuongeza nyengine zaidi, hivyo aliwaeleza waajiri na wakuu
wa taasisi hizo kwamba wanawajibu wa kuwasimamia maofisa wa SNR wanaoshirikiana
kufanyakazi kwa pamoja na kitengo hicho na kueleza kujumu la kitengo ni
kuratibu majukumu yao.
Kitengo cha (SNR) kipo
chini ya Ofisi ya Rais Ikulu, Zanzibar kilianzishwa Februari 27 mwaka
2021.
IDARA YA MAWASILIANO
IKULU, ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment