RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema watendaji wa taasisi za Serikali
wanawajibu wa kutekeleza maagizo na maamuzi yanayotolewa na Serikali kuu katika
kuleta ufanisi wa kuharakisha maendeleo ya nchi.
Dk. Mwinyi aliyasema hayo
alipozindua mwongozo wa uwekezaji Zanzibar wa mfumo wa kielektroniki kwa
Mamkala ya Uwekezaji Zanzibar, ZIPA katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip,
Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi B Unguja leo.
Rais Dk. Mwinyi alisema lengo la
Serikali ya kuzindua mfumo huo ni kuharakisha utoaji wa huduma rahisi kwa
wawekezaji ikiwemo kusajili, upatikanaji cheti cha uwekezaji na huduma nyengine
zinazotolewa na kituo hicho.
“Ni Matumani yetu, mfumo huu
utasaidia kupunguza usumbufu, kuongeza mapato na kupunguza gharama
zinazomlazimu muwekezaji” Alisema Dk. Mwinyi.
Alisema, mfumo huo wa
kielektroniki utaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za ZIPA pamoja na
kuondosha urasimu usio wa lazima na kasi ya utendaji Serikalini.
Aidha, alisema Serikali inaweka
mazingira wezeshi ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini pamoja na kuchukua
hatua stahiki za kuondosha vikwazo vyote vya kisheria na mifumo inayozuia
mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji.
Alisema mfumo huo utarahisisha
ufuatiliaji taratibu zote zinazohusika hadi mradi unasajiliwa na muhusika
kupatiwa cheti chake cha uwekezaji
Dk. Mwinyi alieleza uwekezaji ni
sekta muhimu kwa maendeleo ya nchi katika kukuza uchumi na kuanzisha fursa za ajira,
aliongoza Zanzibar imefungua milango ya uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na
nje kuja kuwekeza nchini ili kuunga mkono juhudi za serikali.
Alisema Serikali inashirikiana na
wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo mashirika ya kimataifa na sekta binafsi
kwa kuhakikisha mazingira salama ya biashara na uwekezaji unaendelea kuimarika
Zanzibar.
“Tunaamini ongezeko la uwekezaji
ni muhimu kwa nchi yetu katika kutekeleza mipango ya Maendeleo ya Kitaifa….”
Alisema Dk. Mwinyi.
Akizungumzia maendeleo ya miradi
ya uwekezaji nchini Dk. Mwinyi alisema kwa kipindi cha miaka miwili Serikali
imesajili miradi 226 yenye thamani ya mtaji wa dola za Kimarekani bilioni 3.5
ambayo inatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 13,500.
Kuhusu sekta ya uchumi wa buluu
Dk. Mwinyi alieleza sera kuu ya serikali ni kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta
hiyo na kueleza mikakati ya uchumi wa buluu imejikita kwenye kuweka matumizi
mazuri ya rasilimali za bahari na kulinda mazingira ya bahari.
Aidha, alieleza hatua za serikali
katika ujenzi wa bandari jumuishi ya Mangapwani Sekta ya mafuta na gesi, usafiri
wa bandari na Miundombinu katika eneo la uchumi wa buluu.
Akizungumza kwenye halfa hiyo,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga
alisema ufunguzi wa mfumo huo utaisaidia Wizara kuitangaza zaidi Zanzibar kimataifa
kupitia sekta ya uwekezaji pamoja na kuleta mapinduzi ya utoa wa huduma bora na
kuharakisha utendaji kwa taasisi zinazotegemeana kufanikisha uwekezaji nchini.
Naye, Mkurugenzi wa Mamlaka ya
Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Sharrif Ali Sharrif alieleza lengo la taasisi hiyo
ni kuwa kitovu cha kutoa huduma bora Afrika Mashariki na Kati.
Mwongozo, huo uliandaliwa kwa
ushirikiano baina ya Serikali na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP), unaelekeza taratibu zote muhimu za uwekezaji na wawekezaji kwa lengo la
kurahisisha na kufanikisha usajili wa miradi ya uwekezaji nchini.
IDARA YA
MAWASILIANO
IKULU, ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment