Habari za Punde

Wizara ya Maliasili na Utalii Kuendelea Kuimarisha Uwiano wa Kijinsia Katika Uhifadhi wa Wanyamapori

 

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Violeth Mlinga akizungumza leo Jijini Arusha  wakati akifungua Warsha ya Wadau kuhusu ushiriki wa Kijinsia katika utekelezaji wa kazi za Uhifadhi.
Mkurugenzi  Mratibu wa Sera na Miradi wa UNDP, Amon Manyama, akizungumza kabla ya kumkabirisha Mwakilishi wa Katibu Mkuu ambapo  amesema ili kuleta matokeo chanya  katika uhifadhi ni lazima kuboresha usawa wa kijinsia kwenye shughuli za kupambana na ujangili.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Violeth Mlinga ( katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na mara baada ya kufungua Warsha ya Wadau kuhusu ushiriki wa Kijinsia katika utekelezaji wa kazi za Uhifadhi

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara unaofadhiliwa UNDP imesema itaendelea kuchukua hatua za kuimarisha uwiano wa kijinsia katika shughuli za uhifadhi wa wanyamapori 

Hayo yamesemwa leo Jijini Arusha na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Bi. Violeth Mlinga wakati akifungua Warsha ya Wadau kuhusu ushiriki wa Kijinsia katika kupambana na ujangili. 

Hatua hii inakuja kufuatia shughuli za uhifadhi kwa kiasi kikubwa kutawaliwa na uwakilishi wa wanaume na kuwepo kwa  mitazamo kuwa kazi za uhifadhi zinawafaa zaidi wanaume kuliko wanawake.

Ameongeza kuwa  tathmini iliyofanyika wakati wa kuandaa Mradi huo ilibainika kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia licha ya kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika shughuli za uhifadhi

 Amesema ili kuleta mapinduzi ya kifikra kuhusu suala hili, Wizara kwa kushirikiana na UNDP  zimeendelea kutoa  uzito unaostahiki katika mapambano ya ujangili na biashara haramu ya nyara.

Katika hatua nyingine, Bi. Mlinga  amesema  takwimu zinaonesha kuwa asilimia zaidi ya 90 ya majangili wanaokamatwa ni wanaume na kwamba suala hili limeendelea kuathiri familia nyingi pindi  wanaume hao wanapokamatwa na hivyo jukumu la kulea familia linakuwa na wanawake

Kwa upande wa Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Wanyamapori,   Elisante Ombeni   amesema suala la usawa wa kijinsia ni miongoni mwa masuala  yanayotekelezwa kupitia kwenye Mradi huo ili kuhakikisha wanawake wanashiriki kwa wingi zaidi katika uhifadhi

Amefafanua kuwa ili kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikia uwiano wake, Wizara imeweka malengo ya muda mfupi, ya kati na mrefu katika kubainisha majukumu ya wadau.

Naye, Mkurugenzi  Mratibu wa Sera na Miradi wa UNDP, Amon Manyama, amesema ili kuleta matokeo chanya  katika uhifadhi ni lazima kuboresha usawa wa kijinsia kwenye shughuli za kupambana na ujangili.

Amesema endapo Tanzania itafanikiwa kuleta usawa huo wa kijinsia itaweza kufikia lengo la 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu “2030 Agenda for Sustainable Development” linalohimiza kuwa usawa wa kijinsia ni muhimu kwa ulimwengu wenye amani, ustawi na uendelevu.

Warsha hiyo imehudhuriwa  na  Maafisa Waandamizi kutoka UNDP, Wawakilishi kutoka WWF, WCS, AWF, PAMS Foundation pamoja na Wawakilishi wa Makamishna wa Uhifadhi kutoka TANAPA, NCAA, TAWIRI, TAWA,

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.