Habari za Punde

CCM hakitowavumilia baadhi ya Viongozi na wanachama wanaoendeleza makundi yasoyofaa ya kuwagawa Wanachama na kutengeneza migogoro majimboni -Mbeto

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, amesema Chama Cha Mapinduzi hakitowavumilia baadhi ya Viongozi na wanachama wanaoendeleza makundi yasoyofaa ya kuwagawa Wanachama na kutengeneza migogoro majimboni.

 

Kauli hiyo ameitoa katika hafla ya kugawa sadaka kwa ajili ya siku kuu kwa wanachama na wananchi wa Jimbo la Pangawe,Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.


Alifafanua kuwa Chama Cha Mapinduzi hakitokuwa na muhali wa kurudia uchaguzi wa viongozi wa jimbo lolote Zanzibar endapo kitabaini kuna baadhi ya viongozi wanaotumia nafasi zao kukumbatia makundi yanayotengeneza migogoro na fitna ndani ya jimbo.


Alisema baada ya kumaliza Uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama wa mwaka 2022, makundi yote ya kutafuta nafasi za uongozi yanavunjwa na kazi inayobaki ni kulinda na kupigania maslahi ya CCM.

 

Mbeto, alisisitiza kuwa kiongozi,mwanachama na kada yeyote anayeendeleza makundi hayo kwa sasa anafanya usaliti kwani madhara yake yanapelekea kudumaza kasi za utendaji za viongozi waliopo madarakani kwa sasa.

 

Alitaka viongozi waliopo madaraka wapewe nafasi ya kuwatumikia Wananchi na itakapofika wakati wa kuwania nafasi hizo kila mwanachama atakuwa na haki ya kuombea na atapendekezwa na Chama kwa mujibu wa sifa na vigezo alivyonavyo.

 

"Natoa angalizo kwa yeyote anayeendeleza makundi ya kujipitisha majimboni kufanya fitna na migogoro ajue kuwa taarifa zake tutazipata na wakati ukifika hatoweza kuvuka salama.

 

Pia nawaahidi Viongozi,wote wa Chama na Serikali wanaotekeleza vizuri Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 kuwa wasiwe na hofu waendelee kumsaidia Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi  kuchapa kazi kwa bidii za kuwatumikia Wananchi",alisema Mbeto.

 

Pamoja na hayo aliwasihi Wanachama wote wa ndani ya Jimbo hilo kuendeleza umoja,mshikamano wa kuimarisha Chama Cha Mapinduzi.

 

Akizungumza utekelezaji wa Ilani ya CCM alisema serikali ya awamu ya nane chini ya usimamizi wa Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi,imeendelea kuvunja rekodi ya kutekeleza kwa kasi miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ya ujenzi wa barabara za kisasa na skuli za ghorofa.

 

Aliitaka miradi mingine kuwa ni pamoja na ukusanyaji mzuri wa mapato kupitia Mamlaka ya kukusanya Mapato Zanzibar (ZRA) na kwamba fedha hizo zitatumika katika kutekeleza miradi ya kijamii.

 

Naye Mwakilishi wa Jimbo hilo Ali Suleiman Ameir, amesema  lengo la sadaka hiyo ni kuirejesha shukrani kubwa kwa Wananchi wa Jimbo la Pangawe, kutokana na juhudi zao za kuimarisha umoja na mshikamano.

 

Alieleza kwamba kwa ushirikiano wao Viongozi wa Jimbo hilo kuanzia kwa mbunge,mwakilishi na madiwani sambamba na uratibu wa Viongozi wa CCM wameandaa sadaka hiyo ya chakula ili kuwafariji Wananchi wao ambao ndio wapiga kura.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jimbo hilo Dadi Juma Dadi, aliwapongeza Viongozi hao kwa ubunifu wao wa kuwapatia mahitaji muhimu ya sadaka ya chakula Wananchi wa makundi mbalimbali ili waweze kushiriki vizuri siku Kuu ya Eid El fitr.

 

Dadi, alisema jimbo hilo lipo salama kisiasa,kiuchumi na kijamii licha ya kukabiliwa na changamoto ya baadhi ya makada kujitokeza kutangaza nia za kugombea nafasi mbalimbali jimboni humo kabla ya wakati wa Uchaguzi uliopangwa kikatiba.

 

Sadaka hiyo iliyogawawiwa kwa makundi matatu ya wananchi ambao ni wazee,watu wasiojiweza na wanachama na wananchi wa jimbo la Pangawe ambapo wamepokea mchele na tende.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.