NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetwaa tuzo ya mshindi wa kwanza kundi la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kuwa na Sera Bora za Usalama na Afya Mahali pa Kazi. (OSH)
Tuzo hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kwenye viwanja vya Tumbaku mjini Morogoro Ijumaa Aprili 28, 2023.
Kilele cha Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi hufanyika Aprili 28 kila mwaka ambapo Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuiadhimisha siku hii, lengo kubwa ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za watu katika sehemu za kazi ambapo kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwakam huu ni “Mazingira salama na afya ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi.”.
“Katika mfuko suala la mazingira salama ya kufanyia kazi kwa wafanyakazi na wanachama wetu ni kipaumbele chetu, ukiangalia hata hapa kwenye banda letu, utaona hata viti wanavyotumia watumishi wetu ni vile vinavyotakiwa kwa mujibu wa OSH.” Alisema Bi. tulipZaida Mahavu, Meneja wa PSSSF Kanda ya Kaskazini.
Akieleza zaidi Afisa Uhusiano Mkuu wa PSSSF, Bw. Abdul Njaidi alisema katika kuhakikisha suala hilo linazingatiwa kikamilifu ofisi zote za PSSSF kote nchini zina masanduku ya huduma ya kwanza (first aid kit) na wheel chairs.
“Lakini pia wanachama nao hatukuwaacha nyuma, kwa wale ambao kutokana na hali yaafya au umri huwa tunawafuata majumbani kwao wakati wa kipiti cha uhakiki wa wanachama.” Alifafanua.
Akihutubia katika kilelecha hafla hiyo, mgeni rasmi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kusimamia masuala ya usalama na afya mahala pa kazi kwa kuwa ni haki ya msingi ya kila mfanyakazi nchini.
Alisema Mhe. Rais Samia amekuwa kinara katika kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inalindwa kwa kuendelea kuimarisha Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA).
Waziri Ndalichako amewataka OSHA kuendelea kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi kuhusu masuala ya usalama na afya mahali pa kazi na kuwahamasisha waajiri kuweka mifumo sahihi ya usalama na afya katika maeneo yao ya kazi na kuendelea kuzingatia sheria na kanuni za usalama na afya sehemu za kazi.
No comments:
Post a Comment