Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kuutunza Mlima Kilimanjaro Mhe.Jafo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ametoa wito kwa Watanzania kuhifadhi na kuuutunza Mlima Kilimanjaro ili uendelee kuinufaisha nchi.

Ametoa wito huo Aprili 04, 2023 bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Same Mashariki Mhe. Anne Kilango Malecela aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali katika kukabiliana na matukio ya uchomaji moto Mlima Kiliamanjro.

Mhe. Jafo alisema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii ina dhamira ya dhati katika kuhakikisha matukio hayo yanakoma.

Alisema pamoja na Serikali kuunda timu ya kufanya utafiti wa matukio ya moto wananchi wana wajibu wa kuacha vitendo vya ukataji miti na uchomaji moto eneo la hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Hai, Mhe. Saashisha Mafuwe, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis alisema Serikali kupitia Taasisi mbalimbali za ndani ya nchi zikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Cha Kilimo cha Sokoine, na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela vinaendelea kufanya tafiti kuhusu suala hili.

Hata hivyo alibainisha kuwa baadhi ya sababu zilizobainishwa kuchangia hali hiyo ni pamoja na kuongezeka kwa wastani wa joto duniani, shughuli za binadamu zisizoendelevu, ukataji wa miti na uchomaji moto misitu.

Napenda kuchukua fursa hii kuhimiza uongozi na wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kuongeza jitihada za kutunza Mazingira ya Mlima huo kwa kudhibiti uchomaji moto ovyo na kuongeza jitihada za kuhifadhi na kupanda miti,” alisema.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Khamis alisema Serikali inahakikisha Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) unaotekelezwa kwenye Wilaya ya Kaskazini A, Unguja na Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika Kuongeza Usalama wa Chakula katika Maeneo kame nchini (LDFS) unaotekelezwa katika Wilaya ya Micheweni, Pemba inakamilika kwa wakati.

Hivyo, alisema tayari Serikali imechukua hatua za kiutendaji kwa kuwataka waratibu wa miradi kitaifa kuhakikisha miradi inakamilika kikamilifu na kwa ubora.

Aidha, naibu waziri alisema Ofisi ya Makamu wa Rais (SJMT) imeendelea kuwasilina na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (SMZ) ili Kusimamamia utekelezaji wa miradi hiyo kwa upande wa Zanzibar ili Miradi hii ikamilike kwa wakati.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Chaani Mhe. Hamad Juma Usonge aliyeuliza

Serikali ina mpango gani wa kukamilisha Miradi ya muda mrefu ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.