Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Wananchi baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Malindi Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameiasa
jamii kuendelea kutekeleza maarisho ya Mwenyezi Mungu na kufuata mafundisho ya
Mtume SAW kwa kufanya yaliyo mema na kuacha mabaya yanayomchukiza Allah (S.W).
Al hajj Dk. Mwinyi alitoa nasaha hizo kwenye Msikiti
Mkuu wa Ijumaa Malindi, Wilaya ya Mjini alikojumuila na waumini wa dini ya
Kiislamu kwenye ibada ya sala ya Ijumaa.
Aliiasa jamii kuchunga familia zao na kuendeleza
malezi ya pamoja badala ya kutelekeza familia kwa visingizio vya talaka,
aliwataka familia wazichunge ndoa zao ili wajenge ustawi wa jamii iliyobora.
“Ndani ya jamii zetu
tuna mtihani mkubwa wa idadi kubwa ya wajane na wanapata shida kubwa ya
maisha” Alieleza Al hajj Dk. Mwinyi.
Alisema wanawake wanaoachika kwenye ndoa zao, sio
tuu huachwa peke yao na waume zao, bali hutwishwa mzigo mzito wa ulezi wa watoto
peke yao, jambo alilolieleza huwasababishia wanawake wengi ugumu wa maisha na kuwa
chanzo cha watoto wengi mitaani kuishi kwenye mazingira magumu.
Al hajj Dk. Mwinyi, alieleza hivi sasa ndani ya
visiwa vya Unguja na Pemba kumeibuka vyama vingi na vikundi vya wajane
waliojikusanya pamoja kupaza sauti zao huku wakiambulia jukumu zito la ulezi wa
watoto peke yao na kuwatunza na kuongeza kuwa watoto wengi wa aina hio hukulia kwenye matatizo mengi.
“Watu wanaacha ovyo bila utaratibu, wanaisababishia
jamii kupata watoto wengi waliotelekezwa, watoto wengi wa aina hii maisha yao
yanakua magumu sana” kwa hisia alieleza Al hajj Dk. Mwinyi.
Hata hivyo, Al hajj Dk. Mwinyi aliwaomba waumini wa
dini kuendelea kuwaombea du’a za kheir viongozi wao kwekwe jukumu kubwa la
kuiongoza, Zanzibar.
Naye, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi
ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, ameitaka jamii hususani wanaume, watatue matatizo yao kupitia mafundisho ya Mtume (SAW)
kwa kusoma sana du’a na kuleta adhkari kwa wingi, badala ya kutoa maamuzi
mabaya yenye athari mbaya kwa jamii.
Akizungumza sheria za talaka
msikitini hapo, khatibu wa ibada ya sala ya Ijumaa, Sheikh Ali Abdulfatah
Yussuf alieleza, talaka ni halali alioichukia mno Allah (S.W).
Pia, aliitaka jamii
kujichunga sana wakati wa utoaji talaka kwa kuzifuata sheria na sunna za talaka
zilizowekwa kwa misingi ya dini pamoja na kujiepusha kufanya maamuzi ya siyo
sahihi wakati wa kutoa talaka kwa wake zao.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment