Habari za Punde

Jamii Yanufaika na Mradi wa Viungo

Mkulima wa Vanila kutoka Kijiji cha Donge Mbiji, Muhidini Zubeir Ameir akielezea kuhusu zao hilo wakati alipotembelewa na waandishi wa habari wakiwa katika ziara ya kuangalia manufaa yaliopatikana kwa wakulima hao kupitia mradi wa viungo chini ya ufadhili wa umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na serikali ya mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo.

WAKULIMA wa mradi wa viungo wamesema kupitia mradi huo wamenufaika na kuweza kuwainua kiuchumi.

Wakulima hao waliyasema hayo wakati walipokuwa wakizungumza na Waandishi wa Habari  katika ziara ya kuangalia manufaa yaliyopatikana kupitia mradi huo  kwenye maeneo mbalimbali ya Unguja.

Walisema hapo awali walikuwa wakilima lakini hawajanufaika, hivyo mradi huo umewasaidia kuwainua kiuchumi kutokana na kuacha kilimo cha mazoea na kulima kilimo bora cha biashara.

Walifahamisha kuwa kilimo hicho kilikuwa sio cha kisasa lakini baada ya kupatiwa elimu imewasaidia kuongeza ubunifu na kuongeza uzalishaji wa mazao tofauti ambayo kwa namna moja au nyengine yamekuwa chachu ya kuwaongezea kipato.

Hata hivyo walisema mradi huo umewakomboa kutokana na kupatiwa elimu, mbegu bora na miundombinu ya maji haliambayo imewasaidia kuwainua katika kilimo hicho.

Mkulima wa matunda na vanila kutoka kijiji cha Kizimbani, Hasne Abdalla Abeid alisema mradi huo umembadilisha katika maisha yake hasa kupitia kilimo cha zao la pesheni ambapo amekuwa akipata soko la uhakika.

Alisema toka kuanza kilimo hicho amekuwa akinufaika kwa asilimia kubwa kwa mavuno ya awamu tofauti, haliambayo imemsaidia kupata tija kutokana na kuweza kuweka ustawi mzuri wa maisha yake.

Alisema licha ya kuwa kilimo cha vanila kinachukuwa siku nyingi kuvuna kwake lakini kilimo hicho kina tija kubwa kwa wakulima wa mradi huo, hivyo aliwataka wasimamizi wa mradi huo kuendelea kuwaunga mkono ili wazidi kunufaika zaidi kupitia sekta hiyo.

Mkulima wa vanila kutoka kijiji chaDonge Mbiji, Muhidini Zubeir Ameir, alisema kilimo hicho hivisasa kimeonekana kuwa na soko hapa nchini na nje ya nchi haliambaayo inasaidia kuwanufaisha wakulima hasa vijana.

Alisema wakulima wa kilimo hicho hususan vijana wanalima kwa ujuzi kutokana na elimu ya waliyopatiwa kupitia wakufunzi wa mradi huo kwa lengo la kuwanufaisha wanawake na vijana katika kujikwamua na maisha yao.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuwataka vijana kuacha kukaa mitaani na badala yake kujishirikisha katika kilimo tofauti kwani eneo hilo litawasaidia kujikwamua na hali ngumu ya maisha na kujipatia kipato kilicho bora.

Mkulima wa mbogamboga na matunda  kutoka Kidimni Soud Mohamed Salum, alisema tangu kupata ujuzi wa kilimo kupitia mradi huo analima kilimo hicho kwa tija zaidi tofauti na hapo awali.

Alisema kwa upande wake mazao ya mboga mboga kwake hayaadimiki kwa wakati wote yeye amekuwa akiendeleza kilimo na kuuza mazao hayo haliambayo hujipatia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yake.

Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuwatembelea mara kwa mara na kwenda kusikiliza changamoto zao ili waweze kuwatatulia kwa wakati na kuendeleza shughuli zao kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.

Alifahamisha kuwa wakulima hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali lakini cha kushangaza serikali haiwapitii na badala yake wanawaona watu wa mradi pekee hivyo hofu yao kubwa kwamba kumalizika kwa mradi huo watashindwa na sehemu za kupeleka kilio chao na kupatiwa ufumbuzi.

Ofisa Biashara na Masoko wa Mradi wa Viungo Zanzibar, Zulfa Bashiri Mbwana alisema mradi huo umelenga kuwawezesha wakulima hao kupata masoko ya uhakika ya ndani na nje ya nchi ili kulima kilimo cha kudumu na kuinua uchumi wao.

Alisema kutokana na hali hiyo imeweza kuwasaidia waakulima hao kuweza kupeleka bidhaa zao katika baadhi ya mahoteli sambambasa na kushiriki katika matamasha mbalimbali ambayo yanawasaidia kujitangaza na kuuza bidhaa hizo.

Alifahamisha kuwa mradi huo upo katika hatua za mwisho kumalizika lakini serikaki itawekeza kupitia eneo hilo kwani itasaidia vijana wengi ikiwemo wanawake kupata ajira kupitia eneo hilo na kuweka mustakabali mwema wa maisha yao.

Mtaalamu wa kilimo katika mradi huo Shaaban Peter alisema wanawaelekeza wakulima hao namana ya kilimo bora ili kupata manufaa ya kilimo hicho.

Akitaja miongoni mwa njia wanazowafundisha alisema kwamba wakulima wanafundishwa kulima kilimo cha umwagiliaji kutokana na hali ya mazingira ya Zanzibar ili kuweza kulima wakati wote.

Alifahamisha kuwa wakulima wamewawezesha kwa kuwachimbia kisima ili kuwapa uhakika wa maji katika kilimo chao.

Ofisa kilimo cha Matunda kutoka katika mradi huo Elibeth Galos Mgawe, alisema wamewaweshesha wananchi hao kutumia mbinu bora za kulima kilimo cha matunda ili kuinua uchumi wao.

Alisema hatua hiyo imesaidia kuleta mabadiliko makubwa kwa wakulima hao kutokana na kuona umuhimu wa kilimo hicho baada ya kuwaongezea kipato na kujikimu katika maisha yao.

Nae Mkuu wa Mawasiliano wa Mradi wa Viungo, Sophia Ngalapi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA ZNZ), alisema mradi huo una malengo makuu manne ikiwemo kufungua fursa ya minyororo ya thamani kwa wakulima wadogo wadogo ambao wanalima mboga mboga,  matunda na viungo kwa Unguja na Pemba.

Alifahamisha kuwa mradi pia unalenga  kuwafikia wanufaika zaidi ya elfu 57 kwa Unguja na Pemba ndani ya kipindi cha miaka minne ikiwa sasa ni miaka mitatu tangu kuanza kwa  mradi huo.

Aidha alifahamisha kwa upande wa Tamwa Zanzibar katika mradi huo wamejikita zaidi kwenye masuala ya mawasiliano na kuutambulisha mradi zaidi kwa jamii na kuuwelewa na kunufaika nao.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi, wakulima hasa wanawake na vijana katika kipindi hiki cha mwisho wa mradi watumie fursa ya mradi wa viungo kwa umakini zaidi kwasababu lengo ni kukifanya kilimo hicho kuwa kilimo biashara badala ya kilimo cha kawaida ili kuinua maisha ya wakulima wadogo wadogo, mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Mradi huo wa viungo unatekelezwa kwa mashirikiano kati ya TAMWA Zanzibar , PDF pamoja na Community forest Pemba (CFP)   chini ya ufadhili wa umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na serikali ya mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo.
Mkulima wa matunda na viungo  kutoka Kijiji cha Kizimbani,Hasne Abdalla Abeid akielezea kuhusu upandaji na ukuaji wa zao la vanila wakati alipotembelewa na waandishi wa habari wakiwa katika ziara ya kuangalia manufaa yaliopatikana kwa wakulima hao kupitia mradi wa viungo chini ya ufadhili wa umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na serikali ya mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo.
Waandishi wa Habari wakiangalia viungo vikiwa katika kiongeza thamani (SOLAR DRYERS) huko Kizimbani Sakafuni wakati wa ziara yao katika mashamba ya  wakulima walioko chini ya mradi wa viungo unaofadhiliwa na umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na serikali ya mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo 
Waandishi wa Habari wakiangalia viungo vikiwa katika kiongeza thamani (SOLAR DRYERS) huko Kizimbani Sakafuni wakati wa ziara yao katika mashamba ya  wakulima walioko chini ya mradi wa viungo unaofadhiliwa na umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na serikali ya mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo. 


Mkulima wa matunda na mbogamboga eneo la Kidimni Soud Mohamed Salum akizungumza na waandishi wa habari kuhusu faida alizozipata kupitia mradi wa viungo unaofadhiliwa na umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na serikali ya mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo  wakati wa ziara ya waandishi hao kwa wakulima walioko chini ya mradi huo katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar.Juni 21,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA MAELEZO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.