Na Khadija Khamis – Maelezo. Zanzibar.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatib Makame amewataka Wajumbe wa Kikosi kazi cha kutokomeza kipindupindu Zanzibar kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Maruhubi, wakati wa kikao cha nne cha kikosi kazi kinachosimamia utekelezaji wa Mpango wa kutokomeza kipindupindu Zanzibar (ZACCEP)
Amesema utekelezaji wa Mpango huo sio nguvu ya sekta moja bali mashirikiano ya pamoja ambayo yatasaidia kufikia malengo ya serikali ya kuhakikisha inayatokomeza maradhi hayo nchini.
Nae Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), nchini Tanzania Andermichael Girlmy amesema ameridhika na kikosi hicho kwa utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo jambo ambalo linasaidia ufanisi.
Amesema amefurahishwa na mashirikiano ya pamoja katika utekelezaji wa Mpango huo kwa sekta mbali mbali hali ambayo inaongeza juhudi za utendaji kazi.
Akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa Mpango huo Afisa Afya kutoka Pemba Khalfani Shaha Bakari amesema elimu mbali mbali zinatolewa kwa jamii juu ya umuhimu wa utumiaji wa maji Safi na Salama pamoja na suala la usafi wa mazingira ili jamii ifahamu visababishi vya maradhi ya mripuko.
Alifahamisha kuwa juhudi hizo zimesaidia kuboresha matumizi ya vyoo vilivyobora kwa jamii ili kupunguza maambukizi ya maradhi ya mripuko.
“Katika kuimarisha juhudi za usafi wa miji na vijiji serikali imeimarisha vikundi vya taka kwa kuwapatia vifaa kinga na vifaa vya usafi kwa ajili ya kazi zao” alieleza Afisa huyo.
Aidha alisema vikundi hivyo vimepewa elimu ya kusarifu taka kuwa bidhaa ili kujiengezea kipato katika vikundi vyao vya ushirika.
Nae Mjumbe wa kikosi hicho Yussuf Matti Ali kutoka Manispaa ya Magharibi B amesema kuwa licha ya juhudi zinazochukuliwa za kutoa Elimu ya usafi wa mazingira kwa jamii bado kuna baadhi ya wananchi bado wagumu kubadillisha tabia zao na kurejesha nyuma jitihada za mpango huo.
No comments:
Post a Comment