Serikali imesema imeandaa hatua na mikakati madhubuti yenye kuibua fursa za miradi ya kijamii kwa wananchi ikiwemo kanuni na mwongozo wa biashara ya kaboni ikiwa ni njia mbadala ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yameelezwa leo Jumatatu (Juni 19, 2023) na Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Abdallah Hassan Mitawi wakati
akifunga warsha ya siku moja baina ya wahariri wa vyombo vya habari na
Menejimenti ya Ofisi hiyo iliyolenga kujenga uelewa kuhusu kanuni na mwongozo
wa biashara ya kaboni.
Mitawi amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi
zinazoathiriwa na athatri za mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa
isiyotabirika hali inayojidhihirisha kupitia matukio ya mvua zisizotabirika,
ongezeko la joto, ukame na mafuriko, ambapo athari hizo zimeathiri sekta za
kijamii na kiuchumi.
“Pamoja na changamoto zinazochangiwa na mabadiliko ya
tabia nchi kumekuwa na fursa na jitihada mbalimbali ambazo zimechukuliwa na serikali
ikiwa ni pamoja na mapitio ya sera, uandaaji wa kanuni, mikakati na miongozo ya
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi” amesema Mitawi.
Akifafanua zaidi Mitawi amesema biashara ya kaboni ni
mojawapo ya nyenzo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi duniani
inayotekelezwa na nchi wanachama wa Maktaba wa Mabadiliko ya tabianchi, itifaki
ya Kyoto na makubaliano ya Paris, ambapo Tanzania ni mwanachama wa mikataba hiyo.
Kwa mujibu wa Mitawi pamoja na kuwepo kwa sera na
mikakati mbalimbali, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Kanuni
na mwongozo wa usimamizi wa biashara ya kaboni ya mwaka 2022 ili kuweka
utaratibu na masharti yanayopaswa kuzingatiwa na wadau na wawekezaji wa biashara hiyo nchini.
“Kanuni na mwongozo wa biashara ya kaboni tayari
zilishatangazwa kupitia Gazeti la Serikali Na. 636 la tarehe 28 Oktoba, 2022 na
hivyo kuwa tayari kwa matumizi. Nyenzo hizi zimejikita katika kuimarisha
mchango wa nchi katika jitihada za kupunguza uzalishaji wa gesi joto” amesema Mitawi.
Akiwasilisha mada kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi,
Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba amesema
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine duniani imeendelea kushuhudia uharibifu wa
mazingira ikiwemo uchafuzi wa bahari, mito na vyanzo vya maji, ukataji wa miti
na upotevu wa bionuai, kuongezeka kwa joto la dunia, mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Komba amesema katika kukabiliana na athari hizo,
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kutumia mbinu mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya
Tabianchi ikiwemo kupunguza uzalishaji wa gesijoto na kuzijengea uwezo jamii kustahimili
athari za mabadiliko ya tabia nchi kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo kilimo cha
umwagiliaji, uchimbaji wa mabwawa na kujenga miundombinu ya kudhibiti mafuriko
na mmomonyoko wa udongo
Akiwasilisha mada kuhusu Mchakato wa Usimamizi wa
Biashara ya Kaboni, Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC)
Prof. Eliakimu Zahabu amesema Mwaka 1997 Umoja wa Mataifa ulianzisha Itifaki ya
Kyoto ambayo ilizitaka nchi zilizoendelea
kupunguza uzalishaji wa gesijoto kwa 5%.
Prof. Zahabu amesema kwa kuzingatia umuhimu wa
biashara hiyo, itifaki hiyo iliweka usimamizi wa biashara ya Kaboni katika
ngazi mbili ambayo ni Ngazi ya kimataifa unayohusisha uaandaaji wa huandaa sera
na miongozo, mfumo au utaratibu wa kimataifa pamoja na ngazi ya kitaifa
inayohusisha Mwongozo na Kanuni za
biashara ya kaboni.
Aidha Prof. Zahabu amesema Kituo hicho imeendelea
kuchukua hatua na mikakati endelevu ya kujenga uelewa kwa jamii kuhusu biashara
ya kaboni katika ngazi zote ili kuvutia wawekezaji na wadau na kuhakikisha kuwa
Tanzania ina inanufaika na biashara ya kaboni kiuchumi sambamba na utunzaji wa
mazingira.
No comments:
Post a Comment