Habari za Punde

Makatibu, Manaibu Katibu Wakuu na Maofisa Wadhamini SMZ wapatiwa mafunzo ya kiutendaji

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe.Zena Ahmed Said akizungumza na Makatibu,Manaibu katibu na Maofisa wadhamini wa Serikali ya Mapinduzi  ya Zanzibar  wakati alipokua akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji  Viongozi hao huko Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar,julai 13,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR
Mkufunzi Profesa Elisante Ole Gabriel akiwasilisha mada ya "uongozi wa kimkakati kwa matokeo makubwa" wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Makatibu ,Manaibu katibu na Maofisa wadhamini wa Serikali ya Mapinduzi  ya Zanzibar yalioandaliwa  na Ofisi ya Rais,Katiba ,Sheria, Utumishi na Utawala Bora na  ya kufanyika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar,julai 13,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR
Baadhi ya Makatibu wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji yakiyoandaliwa na Ofisi ya Rais,Katiba ,Sheria, Utumishi na Utawala Bora na  ya kufanyika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar,julai 13,2023.PICHA NA FAUZIA MUSSA -MAELEZO ZANZIBAR


NA FAUZIA MUSSA - MAELEZO          

KATIBU wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Muhandisi Zena Ahmed Said, amesema kufanyika kwa mafunzo kwa Makatibu wakuu, Manaibu makatibu wakuu na Maofisa wadhamini itasaidia kuwezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi na tija katika Wizara zao.
Akizungumza katika mafunzo ya siku moja kwa viongozi hao, huko katika ukumbi wa Golden Tulip ya Uwanja wa ndege, Mhandisi Zena, alisema, Serikali imeona ipo haja ya kuwapatia mafunzo  viongozi hao ili kuona wanasimamia vyema miradi iliyokuwepo Nchini ya Wizara zao na maeneo yao kwa ujumla.
Alisema, mafunzo hayo yatawawezesha pia kuendelea kufanya kazi zao vizuri katika wizara zao ikiwemo kufuatilia miradi iliyokuwepo kwenye mikakati ili iweze kwenda kwa haraka.
Alisema, miradi mingi ilisimama kwa sababu mbalimbali zilizokuwepo hivyo, kupatiwa mafunzo hayo, wataweza kujua ni namna gani ya kuendelea kuisimamia ili kumalizika kwa wakati.
Mhandisi aliongeza kwa kusema katika kuhakikisha  mafunzo yanafikia malengo yaliyokusudiwa ni lazima  watendaji hao kuwa makini katika mafunzo hayo na kutoa michango mbalimbali panapostahiki.
Akitoa mada ya uongozi wa kimkakati kwa matokeo makubwa, Mkufunzi wa mafunzo hayo, Prof. Elisante Ole Gabriel, alisema, viongozi wa Nchi wanatamani kuona Maendeleo yanaendelea kuwepo katika Nchi na Wananchi wanafaidia kupitia maendeleo yaliyofikiwa chini ya Uongozi wao.
Alisema, ni vyema viongozi hao kuangalia namna gani ya kuwezesha kusimamia fursa zilizokuwepo na kubadilisha changamoto kuwa fursa.
"Hakuna changamoto yoyote iliyokuwa haibadiliki na kuwa fursa, hivyo muende mukabadilishe changamoto zilizokuwepo na muzitengeneze kuwa ni fursa" alisema.
Hivyo, aliwataka viongozi hao kuzigeuza changamoto kuwa ni fursa kwani Rais Dk. Mwinyi, aliwachaguwa kuwa wasaidizi wakuu wa kumsaidia kazi kwa lengo la kufikisha maendeleo kwa wakati.
Nao, viongozi hao, waliahidi kuendelea kutekeleza kazi zao wanazozifanya kwa ufanisi zaidi sambamba na kuendelea kumsaidia Rais katika utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyokuwepo ikiwemo ya mikakati .
Mkutano huo wa siku moja ulioandaliwa na Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora wenye lengo la kuwajengea uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.