Na Faki Mjaka-AGC Zanzibar
Mwanasheria wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji amewataka Wafanyakazi kuiga tabia njema za Wafanyakazi wastaafu ikiwemo kutunza siri za Ofisi ili kujiweka salama wao na Ofisi wanazozifanyia kazi.
Dkt. Mwinyi aliyasema hayo katika hafla ya kumuaga aliyekuwa Katibu Muhtasi wa Ofisi hiyo ambaye amestaafu Bi Masunya Juma Abdalla huko katika ukumbi wa Ofisi hiyo Mazizini mjini Unguja.
Alisema ni jukumu la kila mmoja kuchukua yale mema ambayo wafanyakazi walijifunza kutoka kwake ikiwemo kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na ustahamilivu.
Dkt. Mwinyi alisema Bi Masunya alitanguliza uzalendo na maslahi makubwa ya nchi kwa kuamini kuwa Taasisi anayofanyia kazi ni muhimu ambayo inahitaji mtu mwenye bidii ya kazi jambo lililomjengea sifa ya kuwahi kazini na kuchelewa kutoka siku zote.
Aliwataka wafanyakazi hao kila mmoja kuweka nia na mikakati ya kuhakikisha anaagwa kwa wema kutokana na utumishi wake uliotukuka kama ilivyofanyika kwa Bi Masu.
“Kukusanyika hapa tukafurahia kumuaga mwenzetu ni kwa sababu ya wema wake na utendaji wake uliotukuka, angekuwa Mtu muovu hapa tusingekuwepo hivyo kila mmoja wetu afikirie namna ya kutenda wema zaidi” alisema Mwanasheria Mkuu.
Alimtaka mfanayakazi huyo kutembelea ofisini kila anapopata muda na kutoa ushauri wake ambao anaona unafaa katika kupeleka gurudumu la maendeleo mbele.
Kadhalika Dkt. Mwinyi aliwataka wafanyakazi wa Ofisi hiyo nao kuendelea kumkumbuka na kumtembelea ili kuzidi kuimarisha udugu na uhusiano mwema ambao aliuacha ofisini.
Mwanasheria Mkuu huyo aliwakumbusha Wafanyakazi kuzidisha mapenzi miongoni mwao hasa kwa kuzingatia kuwa maeneo ya kazi ndio sehemu ambayo Mtumishi wa Umma hutumia muda mwingi, hivyo ni muhimu kuwa wastahamilivu na moyo wa kusameheana wao kwa wao.
“Kazini ndio sehemu mnayokutana na kutumia muda mwingi sasa bila kuwa na utaratibu wa kusameheana na kuvumiliana itakuwa ni chanzo cha kugombana na kupelekeana matatizo na mwisho kuharibu kazi” alinasihi Dkt. Mwinyi.
Kwa upande wake Naibu Mwanasheria Mkuu Shaaban Ramadhan Abdalla alisema Bi Masunya aliheshimu na kufuata vyema misingi na maadili ya Utumishi wa Umma kwa kufanya kazi kwa bidii na nidhamu ya hali ya juu kazini.
“Kwa kweli licha ya Umri wake kuwa mkubwa lakini Bi Masunya alikuwa mpole na nidhamu ya hali ya juu, alikuwa anawahi kazini na kuondoka baada ya muda wa kazi, na ilikuwa jambo la nadra sana kuomba udhuru” alimsifia Naibu Mwanasheria Mkuu.
Akitoa neno la shukran Bi Masunya aliishukuru Ofisi hiyo kwa wema wake hasa viongozi kutokana na moyo wa upendo waliomuonesha kipindi chote cha utendaji kazi wake.
Alisema miaka yote 41 aliyofanyakazi alipata mashirikiano mema huku akitoa mfano wa namna mwanawe aliyekuwa Mgonjwa lakini Ofisi hiyo ilishirikiana naye kikamilifu katika matibabu na kumfariji kwa muda wote.
“Katika kipindi kigumu cha kumuuguza Mwanangu ambaye kwa sasa ni Marehemu nilipata kila aina ya ushirikiano, sikupewa maneno makali kwa kukosa kazini baadhi ya siku na kila Mfanyakazi alisimama na mimi katika kunifariji hadi pale mwisho wa uhai wa Mgonjwa” alisimulia Bi Masunya
Hivyo aliwasisitiza Wafanyakazi hao licha ya kufanyakazi kwa bidii wajiwekee mazoea ya kuzidisha kutoa sadaka kwa wahitaji wakiwemo wangonjwa na wajane pale wanaponafasika kwani sadaka huimarisha upendo na kuondoa balaa.
Katika hafla hiyo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ilimzawadia Mstaafu Bi Masunya huyo Shahada ya Utumishi na Vitu tofauti ikiwemo, Mabati, Mifuko ya Saruji na Zulia.
No comments:
Post a Comment