Viongozi wa kikao cha Maafisa Waandamizi wa Sekta ya Afya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiongoza majadiliano ya kikao hicho kinachofanyika katika Makao Makuu ya EAC jijini Arusha tarehe 5 hadi 7 Mei, 2025.
Maafisa Waandamizi wa sekta ya afya kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanakutana jijini Arusha kuanzia tarehe 5 hadi 7 Mei, 2025.
Kikao hiki cha Maafisa Waandamizi kitafuatiwa na kikao cha Makatibu Wakuu wa Jumuiya hiyo kitakachofanyika tarehe 8 Mei, 2025 kwa lengo la kuandaa nyaraka kwa ajili ya Mkutano wa 25 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 9 Mei, 2025.
Mkutano huu wa Maafisa Waandamiz pamoja na masuala mengine utapitia na kujadili taarifa ya utekelezaji wa maamuzi na maagizo ya mikutano iliyopita, na utekelezaji wa programu na miradi ya Vikundi Kazi vitano vya afya katika kanda.
Akitoa salamu za Serikali katika ufunguzi wa kikao hicho, Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe ameeleza ni vema wataalamu wakajikita katika majadiliano ya kitaalam ili kuwawezesha Makatibu Wakuu na Mawaziri kufanya maamuzi yatakayoboresha huduma za afya kwa wananchi wa Jumuiya.
Pia amesisitiza dhamira ya dhati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kushirikiana na Nchi Wanachama wa EAC kuhakikisha sekta ya afya inaimarika katika kanda na kuaainisha baadhi ya vipaumbele ambavyo ni pamoja na; kuhakikisha mifumo ya afya inasomana, kushirikiana katika uchunguzi wa magonjwa ya milipuko na ya kuambukiza, upatikanaji wa teknolojia bora katika huduma za afya na kuimarisha mfumo wa usimamizi wa sekta ya afya.
Naye Afisa Afya Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Erick Nzeyimana kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ameeleza kuwa mkutano huo unafanyika katika kipindi ambacho dunia inapitia changamoto nyingi ikiwemo ya kupungua kwa misaada ya Serikali ya Marekani kwa nchi za Afrika hivyo, ni vema majadiliano ya mkutano huo yakaakisi mahitaji ya Jumuiya pamoja na upatikanaji wa rasilimali fedha kuwezesha wananchi kupata huduma bora na endelevu.
Vilevile, ameeleza baadhi ya jitihada zilizofanyika katika kanda ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa dawa wa uhakika katika kanda, nchi wanachama kutenga bajeti ya kutosha katika miradi ya afya, sambamba na kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ambapo EAC Sekretarieti imesaini makubaliano ya kupatiwa jumla ya Euro Millioni 12 na wadau hao ili kuunga mkono jitihada za kuimarisha huduma za afya kikanda.
Pia ameeleza masuala mengine yaliyotekelezwa ni pamoja na nchi wanachama kuendelea kupata usaidizi katika magonjwa ya mlipuko na huduma tembezi (mobile resources), vituo vya umahiri vimepewa usaidizi ili viweze kutekeleza kikamilifu malengo ya kisekta, mikakati ya udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, magonjwa ya moyo.
Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka akitoa salamu za Serikali katika ufunguzi wa kikao cha Maafisa Waandamizi wa Sekta ya Afya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe. Kikao hicho kinafanyika katika Makao Makuu ya EAC jijini Arusha kuanzia tarehe 5 hadi 7 Mei, 2025.
Sehemu ya ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukifuatilia majadiliano ya kikao cha Maafisa Waandamizi wa Sekta ya Afya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kinachofanyika katika Makao Makuu ya EAC jijini Arusha tarehe 5 hadi 7 Mei, 2025.
Viongozi Waandamizi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakifuatilia kikao cha Maafisa Waandamizi wa Sekta ya Afya ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kinachofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 5 hadi 7 Mei, 2025. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Idara ya Miundombinu ya Kiuchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhandisi Abdillah Mataka, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamin Mkapa - Dodoma na Daktrari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Mkuu wa Matibabu Magonjwa ya Dharura Wizara ya Afya, Dkt. Michael Kilemije.
No comments:
Post a Comment