JAJI Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhan Abdalla, akipata maelezo kutoka mkuu wa Divisheni Idara ya Katiba na Msaada wakisheria Zanzibar Bakari Omar Ali, wakati alipotembelea banda la idara hiyo, akiwa na waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba sheria utumishi na Utawala Bora Dkt.Haroun Ali Suleiman na Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jumanne Sagini, wakati wa Uzinduzi wa Kampenzi ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Na. Maryam Salum. PEMBA
JAJI MKUU wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdalla amesema msaada wa kisheria kwa wananchi ni muhimu sana kwani unachangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa Amani na Utulivu.
Alisema kuanzishwa kwa kampeni ya ya msaada wa kisheria ya mama Samia (MSLAC) utatowa fursa kwa makundi maalum yakiwemo yakiwemo wanawake na watoto nawatu wenye Ulemavu kupata sehemu ya kupeleka changamoto za za kisheria hususan wale wasio na uwezo wa kufunguwa kesi Mahakamani.
Jaji mkuu alieleza hayo huko katika Viwanja vya Bustani ya Mwanamashungi Chake Chake Pemba wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa kusini Pemba katika uzinduzi wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia.
Alisema kuwa anampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kampeni hiyo ambayo inalengo la kuwafanya wananchi wote kupata haki zao jambo ambalo linaonesha uwepo wa haki za binaadamu.
Aliwataka wananchi wa Mkoa wa kusini Pemba kuitumia fursa hiyo kwa kujitokeza kwa wingi katika kupeleka malalamiko yao yanayohusiana na mambo ya kisheria ili waweze kupatiwa msaada wa kisheria ili kuweza kupata haki zao.
Alieleza kama kazi hiyo itafanyika vilivyo itapunguza mrundikano wa kesi kwani kuna baadhi ya migogoro mengine sio ya kuifikisha Mahakamani bali inaweza kutatuka kwa njia ya usuluhishi.
Alifahamisha kuwa anaelewa matatizo yaliomo ndani ya Mahakama ni mingi ikiwemo Mirathi na mali ya amana,Ardhi, na masuala yanayohusiana na mambo ya kadhi hivyo hayo yote yakiwemo kwenye Kampeni hiyo ni vizuri sana kwani ni jambo ambalo limekuwa likileta migogoro.
"Wanapohitaji msaada mkubwa katika kampeni hii ni wanawake na watoto na watu wenye Ulemavu na wengi wao hawana uwezo wa kufikia Mahakamani", alisema.
Jaji mkuu alieleza kampeni hiyo pia itasikiliza mashauri ya Wananchi kwa njia ya Elektronic ili kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.
Kwa upande wake Waziri wa Ofisi ya Rais katiba sheria na Utumishi wa Umma Zanzibar Haroun Ali Suleiman amesema kuwa Viongozi wa nchi zote mbili wamekuwa wakifanya jitihada za makusudi kwa ajili asibakie mtu yoyote wala kuona shida katika kupata haki zao.
Alisema kumekuwa na changamoto mbali mbali kwenye jamii ikiwemo zile za kunyimwa haki kwenye masuala ya Ardhi, na hata kwa watumishi na mengine kama hayo.
" Kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo ndio Viongozi wetu akiwemo Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi kuamuwa kufanya kampeni hiyo ili asibakie mwananchi nyuma katika upatikanaji wa haki," alisema Waziri Haroun.
Aidha kuwataka wananchi katika Mkoa huo kutoka Ushirikiano kwa wale ambao watafika kwenye maeneo yao wakiwapatia elimu ya msaada wa kisheria, ili malengo ya Kampeni hiyo kutoka kwa Viongozi wa nchi yaweze kufikiwa kwa Maendeleo.
Alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa uamuzi wake wa kujenga Mahakama mbali mbali Zanzibar na ndani yake zikiwekwa Ofisi za Wasaidizi wa kisheria.
Hata hivyo alisema Mahakama imejipanga kutengeneza mfumo wa kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jumaane Abdalla Sigiri akitoa salamu za Wizara hiyo aliipongeza Dk Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan kwa kudumisha amani na Utulivu uliozaa Kampeni hiyo kwa maslahi ya watanzania wote.
Alisema huduma hiyo ya msaada wa kisheria imekuwa ni chachu ya upatikanaji wa haki na ni ukombozi kwa watu wasio na uwezo wa kuifikisha mashauri yao katika Vyombo vya sheria ikiwemo Mahakama.
"Kuwepo kwa Kampeni hiyo ya msaada wa kisheria ya mama Samia imehamasisha uwepo wa Amani na upendo kwa jamii kutokana na mashauri mengi kwenda kwa njia ya usuluhishi," alisema Naibu Waziri huyo.
Alifahamisha kuwa Wizara zote mbili za katikaba na Sheria ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar ziliandaa mikakati yakufanikisha suala hilo hususani kwa wanawake na watoto na watu wenye Ulemavu.
Aidha wameandaa mikutano na makongamano ili kifanikisha kampeni hiyo ambayo itawapatia watu wasio kuwa na uwezo kupata haki zao kwa wakati amabazo hapo kabla ya Kampeni wakizikosa.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar Mzee Ali Haji alisema kuwa utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ni mawazo ya Viongozi wakuu wa kitaifa baina yake na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi yakuhakikisha kila mwananchi anaweza kupata haki yake bila uonevu.
Alisema kuwa dhamira ya maono hayo utafikiwa iwapo kila mmoja atatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kushirikiana na wasaidizi wa sheria katika kuielezea changamoto zinazowakabili kwani imeonesha mwanga mkubwa kwa ile Mikoa mabayo umeshaanza Kampeni hizo, ambapo zaidi ya watu 36 elfu wameshafikiwa nchini.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Rashid Hadidi Rashid akitowa salamu za Mkoa huo alisema huduma ya Kampeni ya msaada wa Kisheria ya Mama Samia inqtolewa bure kwa wananchi wote na hii itasaidia uwepo wa Amani na Utulivu na kipato cha mtu mmoja mmoja.
Mkuu huyo wa Mkoa alitoa wito wake kwa wananchi wa Mkoa huo kutoka Ushirikiano kwa wanasheria watakao endesha zoezi hilo ili liweze kufanyika kwa wepesi na vizuri na kwa ufanisi zaidi ili malengo yaweze kufikia.
Aidha aliwataka wanasheria kuwasaidia watu wasio kuwa na uwezo kwa moyo safi ili waweze kupata haki zao bila Changamoto na nimatumaini yake kwamba msaada huo itafanyika kwa njia ya amani na Utulivu hasa Taifa likielekea kwenye Uchaguzi mkuu wa Serikali wa mwaka 2025.
"Wapo wananchi waliowengi hasa wa makundi ya wanawake,watoto na wenye Ulemavu wamekuwa wakikosa haki zao mbali mbali pengine kutokana na kutokuwa na uwezo hivyo kampeni hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa makundi hayo kuweza kupata haki zao kwa mujibu wa sheria,"alieleza Mkuu huyo wa Mkoa.
Kwa upande wake Rais wa Jumuiya ya mawakili Zanzibar Joseph Magaza alisema uzinduzi wa Kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia sio tu kwamba ni usaidizi wa upatikanaji wa haki,Bali ni uthibitishi wa uwepo wa haki za binaadamu Tanzania.
Magaza aliwataka wananchi na wanasheria kuelewa kwamba msaada wa kisheria ni daraja kati haki zilizoandikwa na haki halisi kwani msaada wa kisheria si anasa bali ni haki kwa kupata haki zinazomstakia.
Alisema kila mwananchi bila ya kujali Itikadi na uwezo wake anapata haki ya Ulinzi na mali yake kwa mujibu wa sheria.
Alifahamisha kuwa Kampeni hiyo inalenga kuongeza uwelewa wa kutowa huduma na kuhakikisha hakuna anaebaki nyuma katika kupata usaidizi wa kisheria, ushauri na uwakilishi.
"Jumuiya ya mawakili Zanzibar inalojukumu kubwa na sio kwa wanachama wake tu bali kwa jamii mzima ya Zanzibar kwani majukumu yetu yamejikita katika kulinda utawala wa sheria na kutetea haki na kuhakikisha maadili na weledi katika taaluma ya sheria Zanzibar kama ilivyo ainishwa katika kifungu cha 4 cha sheria cha Jumuiya ya mawakili Zanzibar sheria namba 7 ya mwaka 2019", alisema.
Kampeni hiyo ya msaada wa kisheria ya mama Samia tayari imeshawafikia zaidi ya watu 36 788 wakiwemo wanaume 16992 na wanawake 19866 kwa Mikoa mitatu kwa Zanzibar.
WATENDAJI kutoka Wizara ya
Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora Zanzibar na watendaji
kutoka Wizara ya Katiba na sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
wakifuatilia kwa makini halfa ya Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya
Mama Samia, ilioandaliwa na Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar na
Kufanyika katika viwanja vya bustani ya Mwanamashungi Wilaya ya Chake Chake.(PICHA NA MARIYAM SALIM, PEMBA)
No comments:
Post a Comment