Habari za Punde

UJENZI WA OFISI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE WAFIKIA ASILIMIA 90

Mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki unaoendelea katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, umefikia asilimia 90 huku ukitarajiwa kukamilika Juni 2025. 

Hayo yamebainishwa leo Mei 6, 2025 wakati ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo (Mb.) alipotembelea mradi huo kwa lengo la kujionea hatua iliyofikiwa katika ujenzi huo.

 

Naibu Waziri Londo, akizungumza na Meneja Mradi huo Bi. Ensi Japhet wakati wa ziara hiyo amepongeza hatua iliyofikiwa na amemtaka mkandarasi hilo kuendeleza ubora na kasi uliyopo ili maradi huo ukamilike na kukabidhiwa kwa wakati.

 

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Londo aliambatana na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala Bw. Kawina Kawina na Mhadisi Uyoub Kingunde wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki 

 

Jengo hilo litakalogharimu kiasi cha Shilingi bilioni 22.9 hadi kukamilika kwake, lilianza kujengwa Januari 2022. Ujenzi huo unaogharamiwa na Serikali unalenga kuiwezesha Wizara kuwa na Ofisi ya kudumu katika mji wa Serikali ili kuboresha na kurahishisha utoaji huduma kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.