Habari za Punde

Gesti za Mifugo' mbioni kuanzishwa

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akifafanua baadhi ya mambo wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya sekta ya mifugo nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo jijini Dodoma.
Sehemu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakifuatilia uwasilishwaji wa taarifa ya hali ya sekta ya mifugo nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo jijini Dodoma leo Agosti 24, 2023.

Na Mbaraka Kambona,

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Wizara yake imejipanga kuanzisha gesti za mifugo katika Ranchi za Taifa (NARCO) ili kuwapa fursa vijana na wafugaji wengine kuiweka mifugo yao humo kwa muda maalum ili kuiongezea thamani na kisha kuiuza kwa bei nzuri ndani na nje ya nchi.

Waziri Ulega aliyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya sekta ya mifugo nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo jijini Dodoma leo Agosti 24, 2023.

Alisema Serikali ipo katika mpango wa kuweka miundombinu mizuri ikiwemo majosho na mabwawa ya kunyweshea mifugo itakayowawezesha wafugaji kufanya shughuli zao za  unenepeshaji wa mifugo na kuivuna ili  kukuza kipato chao.

Aliongeza kuwa wataweka utaratibu mzuri wa kuwapata vijana na wafugaji wengine ambao watakuwa tayari kupeleka mifugo yao katika gesti hizo lengo likiwa kuwafanya wafugaji waone tija ya ufugaji wa kisasa na kuondokana na ufugaji wa kuhamahama ambao umekuwa ukiwaingiza matatizoni kila uchao.

Alifafanua kuwa kwa kuanza wataweka miundombinu hiyo katika Ranchi ya Mkata iliyopo Mkoani Morogoro ili kuwapa nafasi wafugaji waliopo katika Bonde la Mto Kilombero waweze kufanya ufugaji wao humo ili waondokane na ufugaji holela.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mhe. David Kihenzile alisema kuwa mpango huo ni mzuri hivyo Wizara ifanye haraka uanze kuutekeleza kwa gharama nafuu huku akiongeza kuwa ni muhimu wizara kuona uwezekano mpango huo kuenea nchi nzima ili vijana na wafugaji wengine waweze kunufaika nao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.