Habari za Punde

Mfuko wa Huduma za Afya kuanza kutumika karibuni

Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa Mfuko wa huduma za Afya Zanzibar Yassir Ameir Juma   akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na mfuko wa huduma za Afya unaotarajiwa kuanza kutumika Oktoba mwaka huu wakati wakipatiwa mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya huduma hiyo.PICHA NA FUAZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR

Baadhi ya Waandishi wa Habari  wakifuatilia mafunzo ya kuwajengea uelewa juu ya mfuko wa huduma za Afya Zanzibar ambao unatarajiwa kuanza kutumika mwezi ujao.PICHA NA FUAZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR

 Na Rahma Khamisi Maelezo Zanzibar   

Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa Mfuko wa huduma za Afya Zanzibar Yassir Ameir Juma   amewataka wafanyakazi wote na wananchi  kujiunga na mfuko wa huduma za afya ZHIF ili kupata huduma bora zaidi nchini.

Akitoa mafunzo  kwa waandishi wa habari kuhusiana na kuanzishwa kwa Mfuko huo huko Michezani Mall amesema mfuko huo utawasaidia wananchi wote bila ya kujali rangi wala  kabila .

Amesema lengo la mafunzo hayo kwa Waandishi  ni kuhakikisha wanakuwa na uelewa kuweza kuelimisha na kushajihisha wananachi kutambua dhamira ya mfuko huo namna utavyowafikia na kuwanufaisha.

"Tunafanya mafunzo haya kwenu nyinyi ili mufikishie taarifa kwa jamii waweze kufahamu  dhana na faida ya mfuko huo na kuweza kujiunga kwa maslahi ya afya na Taifa kwa ujumla.

 Aidha amefahamisha  kuwa  mfuko huo utawasaidia wananchi wote kupata huduma za msingi bila ya kujali vipato vyao na  ni msaada zaidi kwa  wananchi wa kipato cha chini ambao hawamudu gharama za matibabu makubwa.

Katika hatua nyenine Mkurugenzi Mkuu amefafanua kuwa kwa wafanyakazi makato yatakua ni  silimia 7 ambapo  asilimia hizo zitachangiwa kwa mgao sawa kati ya mwajiri na mwajiriwa .

 Aidha aliishauri jamii kuachana na taarifa zizsizo sahihi zinazopelekea kuwa na dhana potofu juu ya mfuko huo na kuwataka kushirikiana katika hilo ili kuleta mageuzi makubwa ya Afya Visiwani.

Mapema Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidhi akifungua mafunzo hayo amesema  lengo la Serikali kuanzisha Mfuko huo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya chini.

Amesema mfuko huo utawasaidia wananchi wa kipato cha chini kupunguza gharama za kufuata matibabu nje ya nchi  hasa maradhi makubwa ikiwemo matibabu ya Saratani ,Figo na huduma za kibingwa.

Aidha amesema kuwa kwa mujibu wa tafiti  iliofanywa asilimia 25.6 ya wananchi hawataweza kuchangia mfuko huo  hivyo Serikali itawachangia ili wapate huduma bora za afya.

Aidha amefahamisha kuwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar limepitisha sheria No 1 ya mwaka 2023 juu ya dhana ya mfuko wa  huduma za afya kwa wananchi  ili waweze kupata huduma bora zaidi.

Naibu Waziri ameeleza kuwa mfuko huo ili uanze kufanya kazi lazima uchangiwe ambapo kwa kuanzia utaanza na  wafanyakazi wa Serikali na baadae Sekta binafsi hadi kuwafikia wananchi wote wa Zanzibar

"kuna kila sababu ya kujipanga na kubuni miundombinu ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ya afya kwa kuanzisha Mfuko wa huduma bora ya afya ili kupata matibabu bora nchini " alifahamisha Naibu Waziri.

Amefahamisha kuwa Serikali inapoteza fedha nyingi kuwapeleka Wananchi wake nje ya Nchi kwaajili ya  matibabu hivyo kuanzishwa kwa huduma hiyo kutasaidia kuzuwia upotevu wa fedha hizo.

Nao washiriki wa semina hiyo wamesema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia katika kuwafahamisha wananchi  kuhusu mfuko huo  ili kuondosha dhana potofu miongoni mwa  jamii.

Mfuko wa Huduma za Afya kwa Wote unatarajiwa kuanza kutumika mapema Oktoba Mwaka huu

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.