Habari za Punde

Ziara ya Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi na PDB Mkoa wa Kaskazini Unguja


Na.Kassim Abdi, WUMU. Zanzibar. 24/08/2023.


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeamua kuzijenga barabara zote zinazoenda katika maeneo ya Utalii Nungwi na Kendwa kutokana na sekta hiyo kuchaingia sehemu kubwa katika uchumi wa Zanzibar.


Viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Ndg.Shomar Omar Shomar kwa kushirikiana viongozi wa Taasisi ya Afisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (PDB) chini yausimamizi wa Meneja miundombinu-PDB Mhandisi John Msemo wameeleza hayo wakati walipofanya ziara ya kuzikagua barabara mbali mbali zilizipo katika eneo la Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.


Wamebainisha kwamba,Kilomita 12.5 za barabara zinazotoa huduma katika maeneo ya utalii zitajengwa katika eneo la Nungwi ili kuondoa changamoto inayowakabili wananchi na wawekezaji wa hoteli katika maeneo hayo.


Wamesema Serikali itaanza kuzijenga barabara zinazoendea katika hotel ya Zalu pamoja na barabara inayoendea katika eneo la uwanja wa ndege wa Nungwi zikifuatiwa na barabara nyengine.


Wamefafanua kuwa Serikali itaanza na barabara hizo kutokana na urahisi wake huku Serikali ikiendelea kufanya tathmini kwa barabara zilizokuwepo katika maeneo ya makaazi ya wananchi ili kuona namna bora ya kuweza kuyaondosha maji kwa kujenga misingi ya kupititishia maji.


Taasisi ya Afisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini wamesema wanafuatilia kwa karibu utekelezaji kutokana na agizo la Mhe. Rais ameshatoa maelekezo ya kujengwa barabara zote zinazokwenda katika maeneo ya utalii katika kiwango bora kwa kuziwekea misingi ya kupitishia maji.


Akitoa ufafanuzi juu ya ujenzi wa barabara hizo Injinia kutoka kampuni ya URKUN Iddy Habibu Mbarouk amesema kampuni inaangalia uwezekano wa kuaandaa na kurekebisha michoro na kuiwasilisha sehemu husika.


Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari imesaini mkataba wa ujenzi wa barabara hizo na Kampuni ya URKUN ikizijumuisha na barabara ya Jumbi - Tunguu, barabara ya Charawe- Ukongoroni- Bwejuu pamoja na barabara ya Bungi ambayo ujenzi wake umekamilika. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.