Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Mwinyi Ameondoka Zanzibar Akielekea Nchini Cuba Kikazi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi akisalimiana na kuagana na Viongozi mbalimbali Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, akiekekea Nchini Cuba, kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la 77 (G 77 + China)  kumuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan.(Picha na Ikulu)   

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi ameondoka Zanzibar kuelekea Havana, Cuba kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la 77 na China (G77+ China) utakaofanyika tarehe 15 hadi 16 Septemba 2023.

Mkutano huo unalenga kukutanisha Mataifa yanayoendelea (Developing Countries) ili kujadili changamoto zinazoikabili dunia hasa baada ya kuathirika na UVIKO-19 na migogoro inayoendelea duniani pamoja na vikwazo mbalimbali vya kiuchumi.  

Hivyo, mkutano huo utajikita zaidi katika kutafuta namna bora ya kujenga ustahimilivu kupitia maendeleo ya sayansi na teknolojia na ubunifu ili kundi la G77 na China liweze kufikia malengo yake kwa pamoja.

Mkutano huu utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Current Development Challenges: The Role of Science, Technology and Innovation”.

Rais Dk.Mwinyi anatarajiwa kuhutubia mkutano huo na kuelezea vipaumbele vya Tanzania, pamoja na hatua zilizochukuliwa kukuza tafiti na kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu (STI) katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.