Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akifanya mazungumzo na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe.Fahad Rashid
Al-Muraikhi, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma tarehe 23
Oktoba 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango leo terehe 23 Oktoba 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Qatar nchini Tanzania Mhe.Fahad Rashid Al-Muraikhi, mazungumzo yaliyofanyika
Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika Mazungumzo hayo Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini ushirikiano
uliopo baina yake na Qatar na imedhamiria kuimarisha na kuendeleza ushirikiano
huo kwa manufaa ya mataifa yote mawili. Makamu wa Rais ametaja maeneo
yanayoweza kuongezwa ushirikiano baina ya Tanzania na Qatar ikiwemo sekta ya Afya,
utafiti wa mafuta na gesi pamoja na biashara ikiwemo bidhaa zinazotokana na
mafuta.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameikaribisha Qatar kuwekeza katika viwanda
vya uzalishaji dawa na vifaa tiba pamoja na kushirikiana katika teknolojia za kukabiliana
na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuwasaidia wananchi kuondokana na matumizi
ya kuni na mkaa na kuimarisha matumizi ya nishati mbadala. Pia amesema Qatar na
Tanzania zinaweza kushirikiana kwenye utalii pamoja na uwekezaji katika
rasilimali watu ikiwemo wataalamu wa afya.
Kwa upande wake Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe.Fahad Rashid
Al-Muraikhi amesema Tanzania na Qatar zinapaswa kuongeza ushirikiano wake ili
kuweza kutumia vema fursa zilizopo katika mataifa hayo. Balozi muraikhi
ameahidi kufanya kazi kwa karibu na serikali ya Tanzania ili kuongeza
ushirikiano katika masuala ya kibiashara.
Kwa pamoja viongozi hao wamejadili namna ya kufanyika kwa ziara za
wafanyabiashara na wawekezaji baina ya mataifa hayo mawili ambazo zitaweza kusaidia
kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo za afya, michezo na
utamaduni.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
23 Oktoba 2023
Chamwino – Dodoma.
No comments:
Post a Comment