Habari za Punde

MAKAMU WA RAIS KATIKA JUKWAA LA NGO'S 2023

 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Kilele cha Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete mkoani Dodoma. (Tarehe 05 Oktoba 2023).

Napenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na siku hii nzuri. Aidha, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima (Mb.), Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kunialika kwenye kilele cha Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Nakupongeza pia kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hapa nchini, pamoja na kufanikisha kufanyika kwa Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa mwaka wa tatu mfululizo.

Vilevile, nalipongeza Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), kwa ushirikiano mzuri na Serikali, hususan katika uratibu wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali hapa Tanzania. Aidha, nawashukuru Wasajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali walioungana nasi katika Jukwaa hili kutoka nchi za Malawi, Ethiopia, Zambia na Uganda.  Karibuni sana Tanzania.

Waheshimiwa Viongozi, Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa;

Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ina jukumu la kusajili na kuratibu shughuli za Mashirika hayo na kuhakikisha kuwa Mashirika hayo yanatekeleza shughuli zake kwa uhuru na kwa kuzingatia sheria, malengo, mipango, mikakati na kwa kufuata misingi ya uwazi na uwajibikaji.

Kimsingi Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yamekuwa yakichagiza jitihada za Serikali katika kuwaletea Wananchi maendeleo kupitia utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali hususan katika afya, kilimo, elimu, maji, mazingira, utawala bora, uwezeshaji wa jamii, miundombinu, mifugo na uvuvi pamoja na sekta nyingine mtambuka. Hakika miradi hiyo, imewanufaisha wananchi wengi kijamii na pia imechangia katika kuboresha utoaji wa huduma mbalimbali, kuongeza  fursa za ajira hasa kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, pamoja na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Nimepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupitia mabanda machache ya maonesho ambayo nimeyatembelea. Nilichokiona ni uthibitisho wa mchango mkubwa unaotolewa na Mashirika hayo katika kuleta maendeleo endelevu kwa Taifa letu. Ninawapongeza washiriki wote wa maonesho haya.

Waheshimiwa Viongozi, Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa;

Serikali, itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yaweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu zaidi. Miongoni mwa hatua ambazo Serikali imechukua katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi na kuongeza utambuzi wa mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, ni pamoja na kuandaliwa kwa Mwongozo wa Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Tanzania Bara (2020), Mfumo wa Kielektroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2020), Kitabu cha Mchango wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Maendeleo ya Taifa (2020/2021/2022), pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (2022/23 – 2026/27).  Hatua nyingine ni uanzishwaji wa Madawati ya Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika Wizara za Kisekta na Mfumo wa Ramani ya Kidigitali ya Utambuzi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs Digital Mapping Tool).

Waheshimiwa Viongozi, Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa;  

Nafahamu kuwa zipo changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiathiri ufanisi wa shughuli zenu. Baadhi ya changamoto kama ilivyoelezwa katika Risala ya Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni uchelewaji wa kupata vibali kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na shughuli mbalimbali, vigezo vigumu vya upatikanaji wa misamaha ya kodi, mifumo ya kielektroniki ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kutosomana na baadhi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutozingatia utekelezaji wa baadhi ya vifungu vya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.

 

Kwa msingi huo, ni vema kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hizo na katika hili, naielekeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kushirikiana na Wizara nyingine pamoja na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kufanyia kazi changamoto hizo. Taarifa ya utatuzi wa changamoto hizo iwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu mapema iwezekanavyo.

Waheshimiwa Viongozi, Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa; Tunapoadhimisha kilele cha Jukwaa hili, napenda kutoa msisitizo maalum katika  masuala matatu ya msingi, kama ifuatavyo:

Kwanza, ni kuhusu uwajibikaji na uwazi katika Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Bado hakuna uwazi wa kutosha kuhusu rasilimali zinazopatikana na namna zinavyotumika katika kutekeleza miradi iliyokusudiwa, na wakati mwingine kuna matumizi ya rasilimali hizo ambayo hayawiani na malengo. Hivyo, nawasisitiza kuzingatia uwazi kwa kuwa ni muhimu katika kuwezesha Serikali kufanya maamuzi mbalimbali yahusuyo uratibu wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, kama vile misamaha ya kodi, michango ya Mashirika hayo katika maendeleo ya nchi n.k.

Pili, ni kuzingatia maadili ya Kitanzania. Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanawajibika kutunza na kulinda maadili kwa kuheshimu mila, desturi na tamaduni za Kitanzania katika utekelezaji wa programu mbalimbali. Aidha, nawakumbusha kuzingatia sheria za nchi na kufuata miongozo mbalimbali inayoratibu shughuli za Mashirika yenu. Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ishirikiane na wadau wengine katika kusimamia suala hili. Tafadhalini sana NGO’s zetu hapa nchini msikubali kuwa tarumbeta za wasiotutakia mema. Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii muendelee kufanya uchambuzi makini wa mchango wa NGO’s na kuishauri serikali ipasavyo juu ya mwenendo na ufanisi wa mashirika haya.

Tatu, ni mabadiliko ya tabianchi. Hili ni eneo muhimu linalopaswa kuangaliwa kwa jicho la kipekee na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hali ya hewa isiyotabirika. Hali hii inadhihirika kupitia mvua zisizotabirika, ongezeko la joto, ukame, mafuriko, magonjwa, ukosefu wa malisho na kutoweka kwa vyanzo vya maji. Athari hizi za mabadiliko ya tabianchi zimeathiri sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kilimo, utalii, nishati, maji, afya, mifugo na mifumo ikolojia ya bahari na ardhi, na hivyo kuathiri ongezeko la pato la Taifa.

Kwa upande wake, Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.  Kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Mikoa na Serikali za Mitaa zimekuwa zikihimiza upandaji miti, kufanya kampeni za usafi wa mazingira na kuhimiza kilimo/uvuvi/ufugaji endelevu unaozingatia kanuni za utunzaji mazingira. Nafahamu kuwa yapo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambayo yanatekeleza majukumu yake katika afua hii ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira. Serikali ingependa kuona ushiriki zaidi wa NGOs katika utoaji elimu na hamasa kuhusu uhifadhi wa mazingira, udhibiti wa majanga na maisha endelevu (disaster management and sustainable livelihood), utunzaji wa misitu na uoto wa asili na kuchangia katika utengenezaji/uboreshaji wa sera mbalimbali. Aidha, mnayo nafasi ya kubuni programu muhimu kama ukusanyaji na urejelezaji taka, biashara ya kaboni, uanzishwaji na utunzaji wa vitalu vya miti na usambazaji wa miche pamoja na usafi wa mazingira katika maeneo maalum, mfano: fukwe za Bahari/Maziwa, barabara n.k.  Nawasihi mshirikiane na Serikali na Sekta Binafsi katika kutekeleza miradi na shughuli mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Waheshimiwa Viongozi, Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa;

Katika Jukwaa hili, tumekuwa na ushiriki wa Msajili wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kutoka nchi ya Uganda. Ninaamini hii ni fursa kwao kujifunza na kuchota maarifa kutoka kwetu namna ambavyo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanavyoratibiwa na yanavyotekeleza majukumu yake. Hivyo, ningependa kuhimiza nasi tujifunze kutoka nchi hizo ili kuboresha uratibu na usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Nawaomba muimarishe ushirikiano huu na nchi zote Jirani nan chi nyingine rafiki katika ukanda huu wa bara la Afrika.

Mwisho, napenda kumalizia kwa kuwapongeza kwa maadhimisho haya ya Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Ni matumaini yangu kuwa utaratibu huu wa kuandaa Jukwaa hili, ambao nafahamu ulipongezwa na kuungwa mkono na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa kilele cha Jukwaa kilichofanyika tarehe 30 Septemba, 2021, utakuwa endelevu.

Baada ya kusema hayo, sasa nipo tayari kwa ajili ya kuzindua mfumo wa Ramani ya Kidigitali ya Utambuzi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kutoa tuzo mbalimbali.

 

Asanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.