Akimnadi mgombea wa Chama Cha Mapinduzi Ndg. Hamad Khamis Hamad wakati wa ufungaji wa kampeni za Chama hicho katika Jimbo la Mtambwe Mhe. Hemed amesema ongezeko la idadi ya wanachama wanaojiunga na CCM kutokea vyama pinzani ni dhahiri kuwa sera na utekelezaji wa Ilani ya CCM vimekubalika ndani ya Jimbo la Mtambwe hivyo wananchi wanayo kila sababu ya kumchagua Mgombea wa Chama cha Mapinduzi ili akashirikiane na viongozi wenzake katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Mtambwe .
Mhe. Hemed amefahamisha kuwa maendeleo yanayoletwa na Serikali kupitia CCM yanawanufaisha wanachi wote ambapo amewataka wananchi kuondoa tofauti zao za kisiasa na kuungana pamoja katika kumchagua mgombea wa CCM akaendeleze mema na mazuri yanayofanywa na chama cha mapinduzi.
Amewataka wanachama wapya na wale wa zamani kushirikiana katika kumuombea kura mgombea wa CCM na kuhakikisha anashinda katika uchaguzi mdogo wa uwakilishi unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 mwezi huu ili aweze kuitekeleza vyema ilani ya CCM sambamba na kuwaletea maendeleo wananchi wake.
Nae mgombea wa Uwakilishi kupitia tiketi ya CCM Jimbo la Mtambwe Ndg. Hamad Khamis Hamad amewaomba wanaCCM na wananchi wa jimbo hilo kumpa ridhaa aweze kuwa mwakilishi wao katika baraza la wawakilishi ili aweze kuwatatulia changamoto zilizobaki Jimboni humo.
Amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe atahakikiasha anaendelea kuitekeleza vyema ilani ya CCM kwa vitendo na atashirikiana na viongozi na wananchi kuhakikisha analeta usawa katika upatikanaji wa maendeleo.
Kwa upande wake Katibu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Salum Suleiman Tate amesema Chama cha Mapinduzi kimefanya kampeni za kistaarabu na kisayansi kwa kutangaza sera Imara zinazotekelezeka na wamejipanga kushinda kwa kishindo katika Jimbo la Mtambwe.
Tate amesema CCCM itashinda bila ya kutumia nguvu kwa vile wapinzani wanajiunga na CCM makundi kwa makundi baada ya kujieone newma zinazoletwa na Rais Dkt Mwinyi.
Mapema Katika ufungaji wa kampeni hizo wananchi kadhaa wa jimbo hilo kutoka vyama pinzani wameamua kujiunga na CCM, hivyo kizungumza kwa niaba ya wanachama wenzake waliojiunga na Chama hicho Ndugu,Salum Abdulla Salum maarufu Daiyadaiya kutoka chama cha ADC amesema ameamua kujiunga na CCM kutokana na kuwa na sera imara, haki na usawa kwa wanachama wote hivyo atahakikisha anashirikiana na uongozi uliopo kwenda kuongeza nguvu katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Amewanasihi wale wote ambao hawajafanya maamuzi ya kuhama upinzani muda bado wanao wa kuzinduka kutoka katika giza totoro na kujiunga na CCM chama ambacho neema zake zimeenea Zanzibar nzima chini ya Rais Makini Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)
Leo tarehe 25.10.2023
No comments:
Post a Comment