Habari za Punde

Amewakumbusha Viongozi wote waliotajwa kwenye Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa mujibu wa vyeo na nafasi zao kuhakikisha wanajaza fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni kuzirejesha Ofisi za Tume ya Maadili si zaidi ya Disemba 31,2023

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewakumbusha viongozi wote waliotajwa kwenye Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa mujibu wa vyeo na nafasi zao kuhakikisha wanajaza fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni na kuzirejesha Ofisi za Tume ya Maadili si zaidi ya Disemba 31 mwaka huu.

Amesema, kuchelewa kurejeshwa fomu kwa wakati bila ya sababu za msingi kwa viongozi hao ni kosa la kimaadili kwa mujibu wa Sheria, hivyo Serikali itawachukulia hatua viongozi watakaochelewa kurejesha fomu hizo.

Dk. Mwinyi ametoa indhari hiyo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu kwenye ukumbi wa Sheikh Idris Abdul Wakil, Kikwajuni, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema, maadhimisho hayo yanatoa fursa ya kujadili kwa kina mustakabali wa nchi, mafanikio ya utekelezaji wa maendeleo kwa ufanisi, kutafakari namna bora ya kuimarisha na kusimamia utawala bora na misingi yake ikiwemo utawala wa sheria, haki, uwajibikaji, uwazi, uadilifu, haki za binaadamu, ubadhirifu wa mali za umma na kupiga vita rushwa.

Alisema, jukumu la kuimarisha misingi ya Utawala Bora si la Serikali na taasisi zake pekee bali ni la wote zikiwemo sekta binafsi, Asasi za Kiraia, Asasi za dini jumuia za kimataifa, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla, wote wanawajibu wa kusimamia na kutekeleza misingi ya utawala bora, kuheshimu na kuimarisha maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, uwazi na kupiga vita rushwa kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.

Alisema katika kuyatekeleza hayo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha taasisi mbalimbali zinazosimamia masuala ya Utawala Bora nchini ikiwemo Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi (ZAECA), Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Tume ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora pamoja na Idara ya Utawala Bora na kila taasisi kupewa majukumu yake ili kuimarisha na kusimamia misingi ya Utawala Bora nchini.

Alisema maendeleo yaliyofanikiwa nchini yamechangiwa kwa uimara na umadhubuti wa taasisi hizo kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka DPP na Mahkama.

Rais Dk. Mwinyi alisema Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma ina jukumu la kusimamia maadili ya viongozi wa umma nchini, kupitia Sheria Na. 4 ya 2015 kwa lengo la kuimarisha misingi ya utawala bora ikiwemo uwazi na uwajibikaji.

Akiizungumzia taasisi ya (ZAECA), Rais Dk. Mwinyi alisema, aliisifu kwa kujenga ushirikiano wa karibu na taasisi za haki jinai zikiwemo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Mahakama pamoja na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama. Ushirikiano huo umeendelea kuleta ufanisi katika kudhibiti wa vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi nchini.

Alisema, kwa kipindi cha utekelezaji kazi Januari hadi Oktoba 2023, ZAECA ilifanikiwa kuokoa fedha kiasi cha Shilingi 2,385,386,720/=. Kati ya fedha hizo, Shilingi 97,944,369/= zilirejeshwa kwa wananchi, Shilingi 2,287,442,351/= zilirejeshwa Serikalini kutokana na makosa tofauti ya rushwa, uhujumu wa uchumi na ukiukaji wa maadili.

Akiiizungumzia Tume ya Maadili kwa mwaka 2022/23, Dk. Mwinyi alieleza kufanikiwa kushughulikia malalamiko 19 na kuyafanyiakazi yakiwemo ukiukwaji wa Sheria ya Maadili dhidi ya Viongozi wa Umma sawa na asilimia 95 ya malalamiko yaliyopangwa ambayo yalihusu maeneo ya matumizi mabaya ya madaraka (15), unyanyasaji (1), uonevu (1), lugha za matusi (1) na kutelekeza familia (1).

Kuhusu Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) alieleza, taasisi hii ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayofanya kazi zake Tanzania Bara na hapa Zanzibar kupitia Sheria Na. 12 ya 2003 ambayo SMZ imeiridhia Tume hiyo kutekeleza majukumu yake Zanzibar.

Alisema kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2023, Tume hiyo imehughulikia jumla ya malalamiko 15, kati ya hayo 13 yalihusu uvunjwaji wa haki za binadamu na mawili ya ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kuitumia Tume hiyo kupeleka malalamiko yao yanayohusiana na uvujifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora ili yafanyiwe kazi na kupatiwa ufumbuzi mwafaka.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa Viongozi waliopewa dhamana serikalini wavitumie vyeo vyao kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazowaongoza, kwani Katiba ya Zanzibar ya 1984 pamoja na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma zinakataza matumizi mabaya ya Madaraka.

Alisema Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu viongozi watakaobainika kuwa makosa, kwa mujibu wa sheria bila ya kumuonea mtu.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Asaa Ahmad Rashid, alisema hatua ya viongozi kuzingatia misingi ya utawala bora inachochea ufanisi wa utekelezaji wa mipango ya serikali kupatikana kwa huduma bora, maendeleo na ustawi wa jamii kwa wananchi.

Aliwakumbusha viongozi wenzake kuhakikisha wanajaza na kuwasilisha fomu zao za mali kwenye Tume hiyo kutokana na viongozi wachache waliorejesha fomu hizo sawa na asilimia 36 ya waliorejesha.

Haki za Binaadamu zinatokana na tamko la kimataifa lililoidhinishwa na kupitishwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Disemba mwaka 1948.

Madhumuni ya Tamko hilo ni kukuza na kuimarisha misingi ya Haki za Binaadamu Duniani. Barani Afrika masuala ya haki za binadamu yamo katika tamko la Afrika la Haki za Binadamu na Watu, (African Charter on Human and People’s Rights).

Tanzania imeingiza masuala ya Haki za Binadamu kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Sura ya Kwanza Sehemu ya Tatu na hapa Zanzibar masuala haya yameingizwa kwenye Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Sura ya Tatu.

Maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu yenye kauli yake Tuimarishe Utawala Bora na Haki za Binaadamu kwa Kuondoa Ubadhirifu na Kukuza Maadili kwa Ustawi wa Jamii” yalilenga kutoa uelewa mpana kwa jamii.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.