Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Amefungua Kituo cha Afya cha Mawasiliano ya Magonjwa ya Mripuko

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka mazingira bora ya kuweza kuepukana na magonjwa mbali mbali ya miripuko sambamba na kuchukua hatua za matibabu pindi magonjwa hayo yatakapojitokeza.

Ameyasema hayo katika Uzinduzi wa Kituo cha Mawasiliano ya Magonjwa ya Miripuko (Zanzibar Afya Call Center) katika Viwanja vya Magomeni - Sogea Zanzibar.

Mhe. Hemed amesema  Sekta ya Afya Zanzibar imekuwa ikichukua hatua mbali mbali katika kuboresha upatikanaji na utowaji wa huduma bora pamoja na kudhibiti magonjwa ya miripuko ambayo yalikuwa  na changamoto kubwa kutokana na kutokuwa na njia bora za mawasiliano kutoka kwa mwananchi kwenda katika Mifumo ya Afya ili kuweza kupatiwa suluhisho la chanamoto hio.

Amefahamisha kuwa Zanzibar ni miongoni mwa  nchi zilizokumbwa na Janga la COVID 19 ambalo lilipoteza maisha ya watu wengi na kuathiri mifumo ya uchumi kutokana na ugumu uliokuwepo wa kusambaza  taarifa kutoka kwa wananchi kwenda  Serikalini juu ya ugonjwa huo.

Amesema kuwa uzinduzi wa kituo hicho cha mawasiliano kitakuwa ni muarubaini utakaorahisisha upatikanaji wa  mawasiliano baina ya wananchi na watoa huduma za Afya pindi magonjwa ya miripuko na dharura yatakapojitokeza sambamba na kuwataka wananchi kukitumia kituo hicho kama kilivyokusudiwa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora na kwa wakati husika.

Aidha Mhe Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwepo kwa kituo hicho kitatoa faida nyingi kwa wananchi ikiwa ni pamoja na mgonjwa kuelekezwa sehemu sahihi ya kupata matibabu kulingana na ugonjwa wake kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Wizara ya Afya .

Sambamba na hayo amesema Kituo cha mawasiliano ya magonjwa ya miripuko kitawasaidia wananchi kufahamu juu ya Mfuko wa wa Huduma za Bima ya Afya Zanzibar ikiwemo namna ya kujiunga, masharti, faida na wanufaika wa amfuko huo pamoja na kuwaunganisha watalii na wageni mbali mbali ambao watapatiwa taarifa za huduma za Afya zinazopatikana hapa  Zanzibar .

Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametoa wito kwa Uongozi wa Wizara ya Afya kuendelea kukitunza kituo hicho kwa kuhakikisha mambo ya msingi yanayohitajika katika kuleta ufanisi wa utowaji wa huduma bora  yanapatikana, kuwepo kwa mafundi watakaotoa msaada wa marekebisho pindi watakapohitajika na kuwa na ulinzi wa uhakika kwa masaa ishirini na nne (24) ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali.

Nae Waziri wa Afya Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema uendeshaji wa kituo hicho unahitaji fedha na nyenzo za kutosha ili kiweze kufanya kazi kwa ufanisi na uweledi wa kuweza kuwahudumia Wazanzibari na wageni wanaoingia nchini kwa wakati.

Mhe. Mazrui amewataka wahudumu wa kituo hicho kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa, Ari na kasi zaidi ili kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya nane (8) inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi  ya kuwatumikia wazanzibar na kutoa huduma bora za afya kwa wote.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka UNICEF Bibi. AWETY ATIE amesema Shirika la UNICEF limekuwa likishirikiana kwa karibu ba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza miradi mbali mbali ya Maendeleo ikiwemo kukikarabati kituo cha Mawasiliano ya Magonjwa ya Mripuko ili kuweza kufanya kazi kwa ufanisi na kupambana na magonjwa ya mripoko yanatotokea nchini.

Amesema UNICEF itaendelea kutoa misaada na mashirikiano kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukiendesha kituo hicho kwa muda wa miaka mitano (5) ambacho kitafanya kazi kwa Mfumo wa kidijitali pamoja na kutoa na kupokea taarifa mbali mbali zinazohusiana na masuala ya Afya.

Aidha Bibi. ATIE amewataka wananchi wa Zanziabar kukitumia kituo hicho pale wanapopatwa na dharura ama kutaka kupatiwa ufafanuzi na ufumbuzi juu ya masuala ya Afya kwa kupiga simu bure kwa namba 190 ama kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba 30 ili kuweza kupatiwa ufumbuzi juu ya tatizo  linalowakabili kwa wakati husika.

Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)

Leo tarehe..13.12.2023

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.