Na Ali Issa Maelezo Zanzibar 21/12/2023.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia,Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma amesema katika jitihada za kumlinda mtoto na ukatili wa kijinsia, Serikali imefanya Mapitio ya Sera na Sharia ya Mtoto ili ziende sambamba na wakati uliopo na mahitaji ya sasa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati alipo kuwa akielezea Mafanikio yaliofikiwa kwa Wizara hiyo ikiwa ni kuelekea kilele cha miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar amesema mpango huo utafanikiwa kwa kuendelea kuzisimamia Sera ya Maendeleo na Sharia ya Mtoto ya Mwaka 2001 na Sharia ya mtoto nambari sita ya Mwaka 2011.
“Ili kuweka utekelezaji bora wa sharia ya kumlinda Mtoto zipo kanuni na sharia zimeandaliwa ambazo ni pamoja na kanuni ya matunzo na hifadhi ya mtoto,makazi na malezi”,alisema Waziri.
Aidha alisema kuanzishwa mazingira ya makazi kwa watoto kupewa huduma za kuwalea watoto na kuwatunza kwa kuhamishiwa jengo jipya la kisasa liliopo Mazizini zitaendelea kwani watoto hao awali walikuwa wanaishi farodhani.
Mbali na hayo alisema kuwa Serikali imefanikiwa kuwapatia Wazee Pensheni jamii , zaidi ya Wazee 29,000 waliotimia umri wa miaka 70 wanapatiwa shilingi elfu 50,000 kitu ambacho kwa nchi za Afrika bado hakija fikiwa.
Hata hivyo Waziri huyo alisema katika kusimamia usawa wa jinsia ,Wizara imeanda sera ya jinsia ya Zanzibar ya Mwaka 2016 pamoja na Serikali kukubaliana na Wadau wa Maendeleo katika kuandaa Sera ya maendeleo ya jamii itayowapatia jamii maendeleo katika Nchi.
Hata hivyo alisema Serikali itaendelea kuwatunza Wazee kwa kuwapatia Makazi bora na salama kwani kila Mtu ni Mzee Mtarajiwa hivyo kuwaekea mazingira mazuri na huduma za matibabu bure ni jambo lamsingi kwani kila mmoja wetu akiendelea kuwa hai basi uzee ajuwe unamnyemelea.
Waziri alitowa wito kwa jamii kuwaunganisha Wazee kwa Masheha waliofikia miaka 70 ili na wao wapate posho linalo tolewa na Serikali.
Hafla ni muendelezo wa vikao baina ya Mawaziri wa Wizara mbali mbali na Waandishi wa Habari katika kuelezea maendeleo, malengo na mafanikio ya Wizara zao, kuelekea Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
No comments:
Post a Comment