Habari za Punde

Wananchi wa Jimbo la Makunduchi Waendelee Kuthamini na Kuunga Mkono Juhudi za Viongozi wa Jimbo

Na.Mwandishi Wetu Zanzibar.

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis,amewasihi wanachama wa Chama hicho katika Jimbo la Makunduchi waendelee kuthamini na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na viongozi wa jimbo hilo.

Hayo ameyasema katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na jimbo kwa lengo la kukutana na wananchi huko Wilaya ya Kusini Unguja.

Mbeto,alisema viongozi hao ambao ni Mbunge jimbo hilo hilo Mhe.Ravia Idarus Faina pamoja na Mwakilishi Mhe.Haroun Ali Suleiman, wanafanya kazi kubwa ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Katika maelezo yake Mbeto,alifafanua kuwa Jimbo hilo limepiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na uwepo wa viongozi imara,wachapakazi na wazalendo wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi,wanaolinda hadhi na historia nzuri ya kisiasa ya jimbo hilo na majimbo jirani.

“Makunduchi ya sasa sio ya miaka 15 iliyopita kwani hivi sasa mnaona kuna kila huduma muhimu zikiwemo Hospitali,Skuli,Ofisi mbalimbali za umma,maji safi na salama pia ujenzi wa barabara za Mijini na Vijijini.”,alisema Mbeto.

Kupitia mkutano huo alieleza kuwa Serikali zote mbili zimeendelea kutekeleza vizuri Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025, kwani siku za hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan baada ya kushiriki katika Mkutano wa Afrika na Saudia Arabia Tanzania imepata fursa ya kupeleka Manesi 1,000 nchini humo.

Pia alisema kutokana na juhudi za Rais Dkt.Samia, zinazotokana na kutangaza Utalii Duniani umeipatia Tanzania heshima ya kuwa nchi ya pili barani Afrika inayoongoza kwa kupokea Watalii wengi.

Pamoja na hayo Katibu alisema kwa upande wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi,anatekeleza kwa vitendo Sera ya Uchumi wa Bluu kwa kuboresha miundombinu ya bandari mbalimbali nchini pamoja na kufungua milango ya uwekezaji hali inayoongeza upatikanaji wa fursa mbalimbali za kiuchumi.

Katibu huyo akifafanua hoja za baadhi ya Viongozi wa vyama vya upinzani kudai kuwa SMZ imeuza bandari ya Malindi, alitaka wananchi kupuuza upotoshaji huo na kueleza kuwa Serikali imeingia mkataba wa biashara na kampuni ya AGL Group ili kuendesha badari hiyo kitengo cha Makontena kwa miaka 5 kuhudumia makasha na kupungua kwa muda kutoka siku 5 hadi masaa 24.

Kupia Mkutano huo aliwakumbusha Wanachama wa CCM kujitokeza na kuwahamasisha Vijana wenye sifa kushiriki katika uhakiki wa zoezi la daftari la kudumu la wapiga kura litakalifanyika hivi karibuni katika jimbo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.