Habari za Punde

SMZ Inaendelea Kuweka Jitihada Kubwa za Kuimarisha Upatikanaji wa Elimu Bora

Na.Maulid Yussuf - Zanzibar  

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe Riziki Pembe Juma amesmea Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuweka jitihada kubwa za kuimarisha upatikanaji wa elimu bora kwa kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Mhe Riziki ameyasema hayo wakati akiweka jiwe la msingi la Skuli ya Msingi ya Kidichi ikiwa ni shamra shamra za sherehe za miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, amesema ujenzi wa Skuli hiyo ni moja wapo ya hatua thabiti katika kutekeleza azma ya ya Serikali ya kuhakikisha visiwa vya Zanzibar vinapata huduma mbalimbali ikiwemo elimu bora na kupata wataalamu wenye uwezo wa kuchamgia maendeleo ya nchi.
Amesema Serikali inatambua changamoto ya Uhaba wa nafasi katika Skuli unaopelekea Skuli nyingi kuendeshwa kwa mfumo wa mikondo miwili kwa baadhi ya Wanafunzi kusoma asubuhi na wengine mchana hali ambayo inakwaza ufanisi katika ufundishaji na kupelekea kudhiofisha maendeleo ya elimu kwa vijana.
Amesema changamoto hiyo inatokana na kasi kubwa ya idadi ya watu, kwani takwimu inaonesha kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita idadi ya wakaazi wa Zanzibar imeongezeka kutoka milioni 1.3 hadi kufikia milioni 1.8 ikiwa ni ongezeko la wastani wa asilimia 3.7 kwa mwaka.
Aidha Mhe Riziki amesema uamuzi wa Serikali wa kuimarisha ubora wa elimu ni sehemu ya mkakati madhubuti katika kufikia malengo yaliyoainishwa katika dira ya Maendeleo ya 2050, ambapo amesema bila ya kuwa na elimu bora inayokwenda sambamba na mabadiliko ya ulimwenguni, itakuwa ni vigumu kufikia malengo ya dira ya 2050.
Amesema uwepo wa jengo hilo la kisasa la Skuli ya msingi Kidichi uwe ni chachu ya kubadilisha mitazamo wa wazazi na walezi kuhusu usimamizi wa elimu kwa watoto ikiwa mwalimu ana jukumu la kutoa taaluma lakini mzazi uwe na jukumu la kutoa ushirikiano kwa walimu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Hata hivyo, Mhe Riziki amesema hayo yote yanafanyika ikiwa lengo ni kumuwezesha kijana wa kizanzibari kushindana vyema katika soko la ajira la Kitaifa, kikanda na kimataifa, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kuhakikisha anawajibika si kwa kuwaandikisha tu watoto skuli bali pia kuwafuatilia kwa karibu maendeleo yao ya kielimu.
Mhe Riziki ametumia fursa hiyo kuwaasa wazazi kuwa karibu Zaidi na watoto wao na kuwafuatilia kwa karibu mienendo yao pamoja na marafiki wao, ili kuwakinga na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto na kusaidia kupata Taifa bora la baadae.
Naye Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Ali Abdulghulam Hussein amesema ujenzi wa Skuli hiyo ni miongoni mwa ujenzi wa Skuli mpya 25 zinazojengwa Unguja na Pemba, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi za kutoa huduma bora za elimu ambapo pia amewahakikishua kuifanyia matengenezo Skuli ya msingi ya Kidichi iliyopo sasa ili iendane na Skuli mpya kwa lengo la kupata elimu bora kwa watoto.
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Naibu Kstibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt Mwanahamis Adam Ameir amesema Skuli hiyo imeanza kujengwa Mei 2023 na inatarajiwa kumalizika mwaka huu na kampuni ya FUCHS na inasimamiwa na ZBA za hapa nchini ambazo ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi. 
Amesema Skuli hiyo ni ya ghorofa 2, ambayo ina madarasa 29, vyoo 25, ofisi 4 za walimu, ukumbi mmoja wa kufanyia mitihani, maabara, chumba kimoja cha Tehamapamoja na maktaba moja, ambapo utagharimu shilingi bilioni 4.5 mpaka kumalizika kwake.

IMEANDALIWA NA KITENGO CHA HABARI NA  UHUSIANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.