RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaagiza
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuendeleza fursa za kuajiri walimu wengi
zaidi wa fani zote ili kuondosha changamoto ya walimu Zanzibar.
Dk. Mwinyi ametoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa
Skuli ya Msingi ya Hamid Ameir iliopo Donge Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa
Kaskazini Unguja ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya sherehe za kutimiza
miaka 60 ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar.
Alisema, kada ya ualimu ni fani muhimu kuliko zote
kwenye sekta za maendeleo, hivyo ameeleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kuboresha mazingira bora ya Elimu kwa kuweka sawa mazingira wezeshi ya
sekta hiyo pamoja na kuimarisha maslahi ya walimu.
Pia, Rais Dk. Mwinyi ameahidi kuongeza uwekezaji
mkubwa kwenye sekta ya elimu kwa kuipa kipaumbele bajeti ijayo ya sekta hiyo
ili kuimarisha mazingira bora kutoka ngazi ya maandalizi, msingi hadi Sekondari
na kuimarishwa vituo vya amali pamoja na kujenga dahalia za kisasa kabla ya mwaka
2025.
Vilevile, Rais Dk. Mwinyi alisema, nia ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kujenga ghorofa hadi skuli za maandalizi na
dahalia ambayo inakwenda kutimia kama ilivyokamilisha skuli ya msingi ya Hamid
Ameir kwa kuwa na madara mengi yaliyopindukia idadi, kuwa na wanafunzi chini ya
idadi ya 45 pia inashuhudiwa kuwa skuli ya kwanza kuwa na mkondo mmoja tuu.
Alieleza hatua hiyo inatarajiwa kuzaa matunda
bora ya matokeo mazuri kwenye kuongeza kasi ya ufaulu mzuri wa wanafunzi.
Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo, kuwasihi
wazazi na walezi kuzitumia skuli hizo kwa kuandikisha wanafunzi wengi zaidi
pamoja na kuiasa jamii kuyatunza na kuyaenzi majengo hayo ili yadumu muda
mrefu.
Akizungumzia miaka 60 ya Muungano baina ya
Tanganyika na Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alisifu hatua za waasisi wa Muungano
huo na wote waliojitolea kuutunza na kuuenzi na kueleza kuwa Muungano wa mfano
Afrika uliodumu muda mrefu sana.
Naye, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Ali Abdul Gulam Hussein alisifu jitihada za Rais Dk. Mwinyi kwa uwekezaji
mkubwa aliowekeza Wizara hiyo.
Alisema, Wizara hiyo tayari imekamilisha
magorofa 20 ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Dk. Mwinyi na
kuahidi kumalizia ujenzi wa skuli za ghorofa kwa majimbo yote ya Unguja na
Pemba kama ambavyo Wizara hiyo imekamilisha kwa baadhi ya majimbo zikiwemo
skuli tano za Mkokotoni, Bumbwini, Tumbatu na Gamba zinazotarajiwa kukamilika
mwezi wa tisa mwaka huu.
Aidha, alieleza Wizara ya Elimu na Mafuzo ya
Amali tayari imeingiza makontena 60 ya vifaa vya skuli mpya zikiwemo meza,
komputa, projekta, mashine za fotokopi, vitanda kwa dahalia zilizokamilika
sambamba na kukamilisha ujenzi wa Dahali tatu kubwa kwa mkoa wa Kaskazini
Unguja kwa maeneo ya Donge, Gambana Bumbwini.
Kwa upande wake Mwakilishi wa jimbo la Donge
ambae pia ni Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano, Dk. Khalid Salum Muhamed alimshukuru
Rais Dk. Mwinyi kwa kufanikiwa kupeleka miradi mingi jimboni humo kiliwemo soko
la kisasa Donge Mtambile, ujenzi wa Daraja kubwa Donge Chechele, kuboresha
barabara za vijini pamoja na kuondosha msongamano mkubwa wa wanafunzi kwa
ujenzi wa skuli za kisasa za Ghorofa.
Katibu mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali, Khamis Abdalla alisema ujenzi wa Skuli ya msingi ghorofa mbili ya Hamid
Ameir uligharimu shilingi bilioni 4.5, umejumuisha madarasa 26, ofisi za
walimu, ofisi ya mwalimu mkuu, vyoo, maktaba, maabara, chumba cha kompyuta na
stoo.
Alisema, skuli hiyo ina wanafunzi 1173 kwa
wastani wa wanafunzi 50, na sasa itakuwa na mkondo mmoja kwa wastani wa
wanafunzi 41 kila darasa moja.
Akizungmza kwenye ghafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa
Kaskazini Unguja, Rashid Hadid Rashid amepongeza juhudi za Rais Dk. Mwinyi kwa
kuinua Sekta ya Elimu Zanzibar.
Alisema, Mkoa wa Kaskazini umebahatika majengo
matano ya ghorofa ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, yakiwemo
majengo ya ghorofa kwa Skuli za Misufini na Makoba kwa Bumbwini Wilaya ya
Kaskazini A, Skuli ya Donge, Mkokotoni na Tumbatu kisiwani.
Pia, Hadid alipongeza jitihada za Dk. Mwinyi
kusambaza vituo vya sayansi (Hubs) kwa mitaala ya sayansi kwa vituo vya
Fukuchani, Mahonda, Kitope, Donge, Bumbwini na Tumbatu pamoja na ujenzi dahalia
kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita na ujenzi wa dahalia ya
ghorofa maeneo ya Gamba.
Akitoa salamu kutoka Chama Cha Mapinduzi, Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya
CCM, Idara ya Itikadi Uenezi na mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis alisema, Ilani ya Chama hicho
ya 2020 – 2025 ndio mkataba baina ya Serikali na wananchi kwa kutekeleza had
izote kwao.
Alisema ilani hiyo imezungumzia masuala ya
elimu kutoka maandalizi hadi vyuo vikuu ambapo kwasasa imepitiliza malengo ya
Ilani hiyo kwa kuongeza ufaulu na kujenga madarasa maradufu hasa kwa skuli za
vipawa vya juu zikiwemo Lumumba kwa Unguja na Fidel kasro kwa Pemba.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment