
Na Ibrahim Dunia. Maelezo.04.04.2024.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Nadir Abdullatif Yussuf Alwardy amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwakumbuka Wazee waliotangulia mbele ya haki na kuleta maendeleo Nchini.
Amesema hayo wakati wa Dua maalum ya kumuombea Hayati Idrissa Abdul Wakil iliyofanyika Makunduchi Wilaya ya Kusini.
Amesema Hayati Idrissa Abdul-wakil ni miongoni mwa Waasisi walioshiriki katika Mapinduzi ya mwaka 1964 hivyo ni vyema kuwakumbuka kwa kuwasomea dua kutoakana na mchango wao walioutoa.
Vilevile amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawaahidi wananchi wa Zanzibar na wanafamilia kuwa itahakikisha itaendelea kujumuika pamoja katika kuwaombea dua na kuwaomba wananchi wa Makunduchi na maeneo ya Jirani kushirikiana nao kwa hali na mali.
"Mimi binafsi ni miongoni mwa matunda ya wazee wetu hawa leo nimekuwa Muakilishi nimekuwa Naibu Waziri na nimepata vyeo vyengine yote haya ni sababu ya matunda ya wazee wetu hawa na tupo huru tunaweza kufanya tunachotaka almuradi tusivunje sheria za nchi" amesema Mhe. Nadir.
Aidha amesema wazee hao wamejitolea na kuwa chachu ya maendeleo yaliopo muda huu kwa kujenga Hospitali, Barabara, elimu yote hayo yametokana na wazee hao walioamua kujitolea kwa hali na mali.
"Mtu yoyote ambae ameamua kujitolea kwenye kuikomboa nchi au kwenye kuleta vitu vyenye neema na manufaa basi ni vyema kumpongeza na kumuombea dua" amesema Mhe. Nadir.
Muakilishi wa Familia ya Hayati Idrissa Abdul-wakil amesema mzee wao alikuwa ni mtu aliyependwa na watu na ameishi nao kwa wema.
Aidha ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kufanya dua hiyo maalum na kusema inapaswa kuendelezwa kwa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Dua ya kumuombea Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Idrissa Abdul-wakil ni miongoni mwa wiki ya kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa ambapo huanzia tarehe mosi April ya kila mwaka na kilele chake kinatarajiwa kufanyika tarehe 07 April, 2024.
No comments:
Post a Comment