Habari za Punde

KONGAMANO LA MIAKA 60 LINATARAJIWA KUFANYIKA TUNGUU ZANZIBAR

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (Centre Foreign Relation) Dkt. Jacob G. Nduye (Kushoto) akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kususiana na Kongamano la Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar litakalofanyika tarehe 30 Aprili, 2024, katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohammed Shein Tunguu Zanzibar.

Na Ali Issa. Maelezo Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussen Ali Mwinyi anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika Kongamano la siku moja la miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, linalotarajiwa kufanyika tarehe 30 mwezi huu katika ukumbi wa Dkt. Shein Tunguu Wilaya ya Kati.

Kongamano hilo litafanyika kwa ushirikiano wa Chuo cha Utawala wa Uma Zanzibar (IPA) na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kilichopo jijini Dar-es-salaam.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari huko Chuo cha Utawala wa Uma Tunguu Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Dkt. Jacob Nduye amesema mjadala huo utafanyika ili kuleta uelewa, ufafanuzi na historia ya safari ya miaka 60 tangu kuasisiwa kwake.

Amesema pia kutakuwa na uchambuzi wa viongozi waliopita kwa awamu nane madarakani kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa awamu ya sita.

Aidha amesema kongamano hilo litahusisha washiriki zaidi ya 1,000 wakiwemo vingozi, wadau mbalimbali, vikosi vya ulinzi na usalama, wanafunzi wa elimu ya juu na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Jumla ya mada mbili zinatarajiwa kuwasilishwa na wanazuoni wabobevu na kujadiliwa na wadau na viongozi wandamizi waliotumika kulitumikia Taifa kipindi kirefu.


Nae Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Utawala wa Uma Dkt. Hamad Khamis Said amesema kongamano hilo litaangalia miaka 60 ya Muungano katika sekta ya uma ambapo jumla ya mada mbili zitatolewa.

Aidha amesema uwasilishaji huo utalenga katika mada ya diplomasia na Uchumi na utawala wa Uma katika kuleta maendeleo endelevu.

Kongamano hilo linadhaminiwa na NMB Bank, Wakala wa Serikali wa Uchapaji, Mamlaka ya udhibiti ya huduma za maji na nishati Zanzibar (ZURA), Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA), Mamlaka ya kukuza uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Drop of Zanzibar, Wizara ya Uchumi wa buluu na uvuvi, Shirika la Bandandari Zanzibar (ZPC) na Viwanda vya idara maaluum za SMZ.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.