Habari za Punde

WAVUVI WAKABIDHIWA MTAMBO WA BARAFU MALINDI

Na.Takdir Ali na Fauzia Mussa. Maelezo. 07.04.2027.

WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Shaaban Ali Othman amesema Serikali inaendelea kutafuta njia mbadala za kutatua changamoto zinazowakabili wavuvi wa Samaki ili kuweza kutekeleza dhana ya Uchumi wa buluu nchini.


Ameyaeleza hayo wakati akikabidhi mtambo wa kuzalisha barafu kwa watumiaji wa soko na diko la Samaki Malindi kutoka kampuni ya Albakora chini ya usimamizi wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu Tanzania.


Amesema mtambo huo  utawasaidia wavuvi wanaotumia diko hilo kwa kuhifadhia samaki wao na kuondokana na adha ya kununua barafu jambo linawasababishia hasara.


Aidha amewahakikishia wavuvi hao kuwa serikali itaendelea kuimarisha huduma za uvuvi  ili  kuweza kufikiwa malengo yaliokusudiwa katika jamii.


Sambamba na hayo ameeleza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kuwasaidia wavuvi wadogowadogo kwa kuwapatia mafunzo yatakayowasaidia kuweza kuvua katika kina kirefu cha maji ya Bahari.


Hata hivyo amewataka wavuvi hao kuutuza mtambo huo ili kuweza kutumika kwa muda mrefu kwa faida yao na vizazi vijavyo.


Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kusimamia Uvuvi wa Bahari kuu Dk. Saleh Yahya amesema mtambo huo umegharimu dola 61  sawa na milioni 100.3 za Tanzania na utazalisha barafu zaidi ya tani tano za vinoo vya barafu kwa siku.


Aidha ameeleza kuwa Kampuni hiyo inawasaidia wavuvi kuondokana na kuvua kwenye maji madogo na kuacha kuvua uvuvi haramu unaoathari nchi.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Albakora kutoka Nchini Spainia Imanol Ioinaz alisema serikali ya Spainia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuleta maendeleo kupiti uvuvi ambapo ameahidi kuwapatia mafunzo ya ubaharia wa uvuvi wa bahari kuu vijana 50 kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

 

Mwenyekiti wa wauzaji samaki soko la Malindi Amour Rashid Amour ameipongeza kampuni ya Albakor chini ya usimamizi wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kupitia Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu Tanzania kwa kuwapatia mtambo huo utakaowaondoshea usumbufu waliokuwa wakiupata kwa muda mrefu  na kuahidi kuutunza na kuutumia kwa matumizi yaliyokusudiwa.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.