Habari za Punde

MAHAKAMA Kuu Zanzibar imetiliana saini mkataba wa ushirikano na Taasisi ya Utawala bora ya Basel kutoka nchini Swizland, juu ya muongozo wa kutaifisha mali zilizopatikana kwa njia ya uhalifu.

Hafla hiyo imefanyika  jana huko Tunguu wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja ambapo Jaji Mkuu wa Zanzibar alisema, lengo ni kutekeleza hayo ni kuhakikisha kuwa uhalifu hauna nafasi hapa Zanzibar.

Jaji Khamis alisema,muongozo huo umekuja baada ya kuzipitia sheria mbali mbali ikiwemo sheria ya dawa za kulevya,sheria ya mwenendo ya makosa ya jinai, sheria ya Kikosi Maalum cha Kuzuwia Magendo, na sheria ya malaka ya kuwia rushwa na Uhujumu Uchumi na sheria nyenginezo.

Alifahamisha kuwa sheria hizo zote zinatoa maelekezo kwamba shauri linapokuja mahakamani lisikilizwe na mshitakiwa anapotiwa hatiani mahakama inaombwa kutaifisha mali alizopatikana nazo.

“Kufuatia mkataba huu tuliosaini ni kuonesha zile taratibu ambazo zitatumika katika kuitafisha hiyo mali”alisema.

Aidha alisema pia wanakusudia kuanzisha mahakama maalum ya makosa ya uhujumu uchumi ambapo taasisi hiyo tayari imeonesha nia ya kuisaidia mahakama hiyo.

Jaji Khamis alisema makubaliano hayo yataongeza nguvu za pamoja kati ya mahakama na taasisi ya Basel, pamoja na kukuza uwezo wa mahakama kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Hivyo alisema Basel kwa pamoja wameona ipo haja ya kuipiga vita rushwa hasa katika mahakama, ambapo kutaleta ushirikiano wa pamoja kama ilivyo katika kurasa nambari 5 ya umoja wa kimataifa ya kupambana na rushwa (UNCAC).

Alieleza kuwa msingi huo unahitaji nguvu ya pamoja kwa nchi kushirikiana katika kukamata, kufiuatilia, pamoja na kurudisha mali zilizoibiwa pamoja na kupambana na rushwa.

Nae Balozi wa Switzerland Didier Chassot ,alisema wameamua kushirikiana na Mahakama kuu ili kuwa na muongozo mzuri ambao utatumika kurejesha mali ambazo zimekamatwa kutoka kwa wahalifu ambao wamekutwa na makosa makubwa.

Alieleza kuwa uhusiano huo umeisaidia mahakama ya Zanzibar kukuza uwezo wake wa kuendesha kesi mahakamani, ambapo makubaliano hayo ni kielelezo ambacho kitasaidia kuleta mageuzi katika mahakama.

Balozi huyo alisema kufanya hivyo ni kuisadia mahakama ya Zanzibar kufikia malengo yake ya kuhakikisha makosa kama  uhujumu uchumi yanapungua au kuondoka kabisa.

Alisema muongozo huo utawasaidia mahakimu, majaji pamoja na wendesha mashitaka pamoja na polisi katika kukamata na kuleta mahakamani kwa kujumuisha makosa mbali mbali ya jinai.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.