Na Khadija Khamis- Maelezo, Zanzibar 28/04/2024.
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa
amesema jumla ya watuhumiwa 251 wamekamatwa kufuatia
operesheni maalum ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu
hapa Nchini.
Ameyasema hayo huko katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa Mjini Magharibi Vuga wakati akizungumza na
waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali.
Amesema watuhumiwa waliokamatwa 22 wamekamatwa na
mapanga na vifaa vya kuvunjia nyumba, 20 wamekamatwa
kwa makosa ya unyan’ganyi, kujeruhi na kushambulia, 6 kwa
makosa ya wizi wa pikipiki wakiwemo mafundi wa pikipiki
wanaopokea mali za wizi na watuhumiwa 203 wamekamatwa
kwa makosa ya uzembe na ukorofi.
Aidha, amefahamisha watuhumiwa wote waliokamatwa katika
operesheni hiyo watafikishwa katika vyombo vya sheria na
majalada yao yemeshafunguliwa kwa ajili ya kufikishwa katika
Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ili kuendelea na taratibu
nyengine za kisheria.
Mkuu wa Mkoa huyo amesema operesheni hizi zitakua
endelevu katika maeneo mbali mbali ya Mkoa wa Mjini
Magharibi hadi kuhakikisha makundi hayo ya vijana
wanaotumia silaha za jadi yamedhibitiwa kabisa kwa
mashirikiano ya jeshi la polisi na vyombo vyengine vya ulinzi.
Pamoja na hayo, Amewaasa vijana ambao wanajiingiza katika
matendo hayo kwamba Serikali haitoacha vitendo hivyo
viendelee itapambana hadi kuhakikisha makundi haya
yanatokomea.
“nitoe indhari kuwa Serikali ya Mkoa pamoja na Jeshi la Polisi
halitakuwa tayari kumuachia kijana yoyote yule atakaebainika
kujihusisha na vitendo vya kihalifu, ”amesema Mkuu wa
Mkoa.
Amewataka wananchi waendelee kushirikiana na vyombo vya
ulinzi hasa hasa jeshi la polisi kwa kuwapa taarifa sahihi za
vikundi vya watu ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo
vya uhalifu katika maeneo yao ili kuweza kudumisha amani na
utulivu kwenye mkoa.
Nae Mkuu wa Wilaya Magharibi ‘B’ ambae pia ni Kaimu wa
Wilaya ya Magharibi ‘A’ Hamida Mussa Khamis
ameishukuru Kamati ya Usalama wa Mkoa kwa kuendelea
kuzisimamia Wilaya zao na kutoa muongozo wa
jinsi ya kukabiliana na uhalifu huo.
Akielezea wilaya yake amesema kuwa bado kumekuwa na
changamoto kwa baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa na
vikundi vya uhalifu ikiwemo Kinuni Kwarara Hawai pamoja
na Mchikichini.
Kwa upande wa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
ACP Richard Thadei Mchomvu amesema operesheni huo
imefanyika kwa aina yake jambo ambalo limesaidia kuleta
mafanikio ya kuwakamata wahalifu.
Hata hivyo amewapongeza masheha na wananchi kwa
mashirikiano yao waliyoyatoa jambo ambalo limeweza
kufanikisha zoezi hilo
Mali zilizookolewa katika Operesheni hizo ni pikipiki 14,
Televisheni 4 , simu 16, mifuko ya saruji 4, Tiles box 5, Viatu
vya raba pair 6 , pasi za umeme 3, frame 44 za pikipiki aina ya
klick na vespa pamoja na N’gombe 2.
No comments:
Post a Comment