Wahasibu wanawake Tanzania wametakiwa kuweka mikakati Imara na thabiti ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii na Taifa kwa ujumla ili kuweza kutanua wigo mpana wa kuhamasisha usawa na haki kwa wanawake na wasichana Tanzania.
Hayo yamesemwa na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. HEMED SULEIMAN ABDULLA wakati akifungua Kongamano la Saba(7) la Uongozi la Wanawake Wahasibu Tanzania kwa Niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Hafla iliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Amesema wahasibu wanawake wana fursa ya kujenga mtandao Imara wa kusaidiana na kuhamasishana kufikia maendeleo waaliokusudia hasa katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Rais Dkt. Samia amesema Serikali itaendelea kuwa washirika wa kimkakati na kusimama pamoja na TAWCA katika kuboresha mazingira ya kazi, kuwekeza katika elimu, fursa sawa za maendeleo pamoja na kuondoa vikwazo dhidi ya wanawake kwa kuwaandaa kuwa viongozi wa kesho wanaotokana na wanawake wahasibu nchini.
Aidha Dkt Samia amesema kuwa TAWCA imekuwa mstari wa Mbele katika kuwainua wajasiriamali kwa kuwapa taaluma za kifedha na stadi za maisha ili kuweza kuyafikia malengo waliojiwekea katika biashara zao.
Dkt Samia amekipongeza chama cha wahasibu wanawake Tanzania kwa shuhuli mbali mbali wanazozifanya ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya biashara na ujasiriamali kwa wanawake, kuwasaidia wahasibu wachanga kuweza kufanya vizuri katika fani zao kwa kuwakumbusha kuzingatia maadili ya kazi zao.
Sambamba na Hayo ametoa wito kwa wadau mbali mbali kuunga mkono juhudi za Serikali kusaidia upatikanaji wa kundi bora la wanawake lenye kujitegemea katika kuboresha na kuinua uchumi katika jamii na Taifa kwa ujumla.
Nae Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe Juma Makungu Juma amesema Serikali inatambua mchango wa wanawake wahasibu nchini katika kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na uaminifu mkubwa hivyo itaendelea kufanya kazi kwa karibu na TAWCA ili kufika malengo ya kuanzishwa kwa Chama hicho.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la TAWCA, CPA Neema Kiure amesema lengo la kongamano hilo ni kuwajengea uwezo na kupeana taaluma na ujuzi kwa wahasibu wanawake ili kuchochea mabadiliko ya kiutendaji na kimaendeleo katika kada ya uhasibu nchini.
Amesema TAWCA imekuwa ikitoa elimu kwa wajasiriamali wanawake juu ya kutunza kumbukumbu za biashara na namna ya matumizi mazuri ya mikopo wanayopatiwa ili waweze kupata matokeo yenye tija na faida zaidi.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa wahasibu na Wakaguzi wa hesabu Tanzania(NBAA) CPA Pius Maneno amesema taaluma ya uhasibu inakuwa kwa kasi Tanzania ambapo hadi kufikia mwaka 2024 wahasibu wanawake waliosajiliwa wamefikia asilimia 34% na ambao wanasaidia kufikisha elimu ya utunzaji wa fedha kwa wafanyabiashara na wajasiri amali nchini.
CPA Maneno amesema kazi kubwa inayofanywa na TAWCA ni kudhibiti na kusimamia taaluma ya uhasibu kwa kuwapatia ujuzi na nyenzo wahasibu wanawake za kuweza kuwafikia wanawake na wasichana nchini kuwapa elimu ya biashara na ujasiriamali ili kujikwamua kimaisha.
Imetolewa na Kitengo Cha Habari ( OMPR)
Leo tarehe ..04 / 09 / 2024
No comments:
Post a Comment