Na.Fauzia Mussa -Maelezo Zanzibar.
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imezindua vitalu viwili vipya vya uwekezaji vya mafuta na gesi asilia katika maeneo ya nchi kavu.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Shaaban Ali Othman akizungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali katika hoteli ya Verde kuhusiana na tukio hilo alisema, hatua hiyo inaenda sambamba na dira ya maendeleo ya Zanzibar 2050, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, Mpango wa Maendeleo ya Zanzibar (ZADEP 2021-2026) na Sera ya Uchumi wa Buluu 2022.
Alisema vitalu hivyo vipo Unguja na Pemba jambo ambalo linaelekeza kuendeleza shughuli za utafutaji wa nishati ya mafuta na gesi asilia hapa nchini kwa kushirikiana na Kampuni za kimataifa za mafuta na gesi asilia (IOCs).
Waziri huyo alisema kufuatia hatua hiyo Serikali inatarajia kupata makampuni mengi ya uwekezaji kwa ajili ya utafutaji na uchimbaji wa nishati hiyo ili kuendeleza rasilimali hizo kwa njia endelevu.
Aliwataka wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta hiyo kufanya maombi ili kuingia mikataba ya kuwekeza ndani ya vitalu hivyo.
No comments:
Post a Comment