RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj
Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema viongozi wana wajibu muhimu wa kuhubiri amani na
umoja kwa kutamka mambo mema ili kuepuka kuleta mifarakano kwenye jamii.
Alhajj Dk. Mwinyi ametoa tamko hilo akitoa salamu kwa waumini
wa dini ya kiislam kwenye ibada ya sala ya ijumaa masjid Baaruut, Mwembe
Mchomeke, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema, viongozi wa dini na wanasiasa wanakila sababu ya kutokuwa
sehemu ya kuvuruga amani kwani kauli zao zinasikika na walio wengi nakuwa na
nguvu hivyo ni vema wakawa mstari wa mbele kuhubiri amani, umoja na mshikamano
kwenye jamii.
Alhaji Dk. Mwinyi amesisitiza kuwa ili nchi iwe na mazingira
mazuri ya kuleta maendeleo kila mmoja kwa nafasi yake hususani viongozi,
wanalazimika kutamka kauli zenye kujenga, kuleta umoja na mshikamano kwani bila
ya mambo hayo nchi haiwezi kupiga hatua kwenye maendeleo.
Akizungumzia suala la malezi na maadili, Al hajj Dk. Mwinyi,
amewasisitiza wazazi na walezi kuwaonya na kuwakemea watoto na vijana pale
wanapofanya mambo kinyume na maadili, silka za tamaduni.
Alisema, dunia ina mabadiliko mengi yanayowaharibu watoto,
ikiwemo utandawazi, matumizi ya dawa za kulevya, wizi na ubadhirifu wa mali za
umma, hali inayotaka mkazo maalum kwa kuhimiza maadili mema na kuwakataza
watoto ili kurudi katika maadili mema na misingi ya uislam.
Akihutubu ibada ya sala hiyo, Khatib sheikh Ahmeid Khamis
Bilali amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwa na uwezo wa kuwamiliki watoto
katika nji nzuri za malezi,
yanayozingatia maadili ya dini ili kuirejeshea Zanzibar sifa na hadhi yake ya
kuwa nchi yenye maadili mema.
Naye, Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid
Mfaume amesema wazazi na walezi wanawajibu wa kuweka utaratibu maalumu wa
kuwahoji watoto ili kujua mambo wanayokabiliana nayo kwa dhamira ya kuwajenga mapema
kwa Imani na maadili.
Aidha, ameihimiza jamii kuunganisha nguvu ya pamoja kwani
suala la malezi sio la mtu au taasisi moja kwani lazima watoto wafundishwe
tawhid kwa dhamira ya kumjua Mola wao.
Amesisitiza kuwa zawadi nzuri zaidi anayopaswa mzazi kumpa
mtoto wake ni malezi bora, elimu na adabu ili nchi iwe na watu wenye nidhamu na
hatimaye kuwa na Taifa bora.
No comments:
Post a Comment