Habari za Punde

TIRA kuunga mkono katika kufanikisha Shereha za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar,

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akipokea mfano wa Hundi ya Shilingi Milioni Mia Tatu na Ishirini na Moja (321) za Kitanzania  kutoka kwa Uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kuunga mkono katika kufanikisha Shereha za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, hafla hio ya Makabidiano ilifanyika Ofisini kwake Vuga Jijini Zanzibar. 

Imetolewa na Kitengo cha Habari(OMPR)

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa kuona umuhimu wa kutoa mchango wao katika kufanikisha sherehe za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Ameyasema hayo ofisini kwake Vuga wakati aliopokutana na Uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) uliofika ofisni hapo kwa ajili ya kukabidhi mfano wa Hundi ya Shilingi za Kitanzania milioni Mia tatu na Ishirini na Moja (321) walizoahidi kuchangia kwa ajili ya sherehe za Mapinduzi.

Mhe. Hemed amesema  fedha hizo zilizotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania ( TIRA ) zitasadia kwa kiasi kikubwa  katika kufanikisha sherehe za Mapinduzi zinazotarajiwa kufanyika Januari 12 katika Uwanja wa Mpira Gombani kisiwani Pemba.

Amesema makampuni mbali mbali yanaendelea kuekeza Zanzibar jambo ambalo linatoa fursa kwa TIRA kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na makampuni hayo katika kuhakikisha wanakata Bima stahiki kwa ulinzi wa mali zao kulingana na uhitaji wa kampuni

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameyasukuru makampuni ya bina kuendeea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na viongozi wakuu wa nchi katika kuwaletea maendeleo wananchi wa pande zote mbili za Muunganio.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais amewahakikishia TIRA kuwa Serikali itaendelea kutoa kipaombele kwa Sekta binafsi katika masuala ya uwekezaji pamoja na  kampuni  wazawa kupewa kipaombele katika miradi ya Serikali lengo ni kuleta maendeleo endelevu nchini.

Makamu wa Pili wa Rais ameyakaribisha Makampuni ya Bima Tanzani kushiriki katika Sherehe za Mapinduzi ikiwemo uzinduzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi katika miradi hiyo pamoja na kuzitumia sherehe hizo katika kutangaza kazi zinazofanywa na  makampuni yao.

Akikabidhi Mfano wa Hundi ya zaidi ya Shilingi za Kitanzania Milioni Mia Tatu(300) Naibu Kamishna wa TIRA Zanzibar  Bi KHADIJA ISSA SAID amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania imefarijika sana kuona imekamilisha ahadi waliyoitoa ya kuchangia katika kufanikisha maadhimisho ya shereha za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar  na kusema kuwa TIRA itaendelea kushirikiana na Serikali katika kufanikisha shughuli mbali mbali za maendeleo kiuchumi na kijamii.

Bi Khadija amezishukuru Serikali za SMT na SMZ kwa kuwapatia ushirkiano mkubwa katika utekelezaji wa kazi za Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania jambo ambalo linawapa msukumo wa kufanya kazi kwa juhudi na kizalendo ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mwenyekiti  wa Umoja wa Makampuni ya Bima Tanzania ambae pia ni Mkurugenzi wa Bima CRDB Bwana NELSON MNZAVA amesema Uongozi wa TIRA umechukua juhudi kubwa kuona kwamba wanatimiza ahadi yao waliyoitoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuahidi kuwa utaratibu huo wa kushiriki katika sherehe za Mapinduzi utakuwa endelevu kwa kila mwaka na kwa kadiri hali itakavyoruhusu.

Mnzava ameziomba Serikali kuwasaidia katika kuzishajihisha Taasisi za Serikali, Taasisi binafsi na Makampuni mbali mbali  kujenga tabia ya kukata bima ili kuziweka kampuni na mali zao katika mazingira salama.

Imetolewa na Kitengo cha Habari ( OMPR )

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.