Habari za Punde

Dkt.Biteko Awasili Nchini India kwa Ziara ya Kikazi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (kulia) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Indira Gandhi, jijini New Delhi nchini India kwa ajili ya kuhudhuria mikutano mbalimbali ya kimataifa kuhusu nishati.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt.Doto Biteko akikaribishwa nchini India na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mafuta na Gesi India, Sandeep Jain mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Indira Gandhi katika Jiji la New Delhi kwa ajili ya kushiriki mikutano mbalimbali ya kimataifa kuhusu nishati.

Kushiriki Mikutano ya Kimataifa na Wiki ya Nishati ya India 

Mawaziri wa Nishati, Watunga Sera na Wavumbuzi wa teknolojia za Nishati kukutana

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo Februari 11, 2025 amewasili nchini India kwa ajili ya kushiriki mikutano mbalimbali ya kimataifa ya nishati ambayo inaenda sambamba na  Maadhimisho ya Tatu ya Wiki ya Nishati ya India mwaka 2025 (India 3rd Annual  Energy Week)  kuanzia tarehe  11 hadi 14 Februari,  2025.

Katika Uwanja wa Kimataifa wa Indira Gandhi, jijini New Delhi,Dkt.Biteko amepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mafuta na Gesi India, Sandeep Jain.

Wiki ya Nishati India itakutanisha Mawaziri na Watendaji Wakuu wa Sekta ya Nishati kutoka maeneo mbalimbali duniani,  watunga sera na wavumbuzi wa teknolojia mbalimbali za kisasa za nishati kwa lengo la kuja na mustakabali endelevu wa upatikanaji nishati.

Aidha, Wiki hiyo itahusisha pia maonesho ya teknolojia mbalimbali za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Katika ziara hiyo, Dkt.Biteko ameambatana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi zake wakiongozwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.