Habari za Punde

SERIKALI YATAKA UWAZI NA HAKI KATIKA MIKATABA YA FEDHA

Baadhi ya wajasiriamali na wananchi kutoka Kata ya Sumve, Malya na Hungumalwa Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, wakiwa pamoja na Timu ya Wataalamu wa Elimu ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake Wilayani humo, wakichangia mada mbalimbali kuhusu elimu ya fedha waliyoipata kupitia  njia ya filamu yenye maudhui kuhusu matumizi sahihi ya fedha, umuhimu wa kupanga bajeti na kuitekeleza, umuhimu wa kusajili vikundi vya huduma ndogo za fedha , utunzaji wa fedha binafsi, umuhimu wa kushirikisha familia na watu wa karibu kwenye masuala ya fedha na uwekezaji, umuhimu wa kukata bima ya biashara na mali nyingine.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WF, Mwanza)

Na Chedaiwe Msuya, WF, Mwanza

Serikali imezitaka Taasisi za Fedha zilizosajiliwa kutoa huduma ya mikopo, kuto wakandamiza wananchi katika mikataba kwa sababu ya kutojua kusoma na kuandika kwa kuwasainisha mikataba bila uelewa wao.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Mkoa wa Mwanza, Mhe Ng’wilabuzu Ndatwa Ludigija, alipokutana na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake, ambayo ipo mkoani Mwanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali.

“Serikali imesisitiza umuhimu wa uwazi na haki katika mikataba ya kifedha ili kulinda haki za wananchi na kuhakikisha wanajua kikamilifu masharti wanayokubaliana nayo”, alisema Mhe. Ludigija.

Alifafanunua kuwa Serikali inatambua kuna baadhi ya wananchi hawajui kusoma na kuandika, wamekuwa wakiwekewa miezi mingi zaidi ya marejesho tofauti na walivyokubaliana kwa mdomo.

Mhe. Ludigija, amewashukuru wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kufika mkoani Mwanza kutoa elimu ya fedha kwa kuwa itawasaidia wananchi kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwemo kupanga bajeti na kufanya uwekezaji ambao utakuwa na faida kwa kujikwamua kiuchumi.

Afisa Mkuu Mwandamizi, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, aliwasisitiza wananchi kujenga mazoea yakusoma mikataba na kuuelewa kabla ya kusaini.

Aliongeza  kuwa baadhi ya wanufaika wa mikopo wanakumbwa na changamoto za marejesho kwa sababu ya kukosa mipango thabiti ya matumizi ya fedha wanazokopa, na wengine hawasomi wala kuelewa mikataba wanayoingia.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha, mkazi wa Kwimba, Bw. Nkwadi Joseph aliishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwaletea wataalamu wa fedha. 

"Kabla ya kupata elimu hii, tulikuwa tunaingia kwenye mikopo yenye masharti magumu bila kujua athari zake, sasa tunaelewa umuhimu wa mikopo yenye utaratibu mzuri," alisema Bw. Joseph.

Serikali kupitia Wizara ya Fedha imefanya hitimisho ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Wilaya za Ilemela, Magu, Misungwi na Kwimba Mkoa wa Mwanza, ambapo hadi sasa Wizara ya Fedha imeshatoa elimu ya fedha katika mikoa 16.

MWISHO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.