Habari za Punde

TANZANIA NA ZAMBIA ZAKUBALIANA KUIMARISHA MPAKA WA KIMATAIFA


 Viongozi wa timu za wataalamu wa Kamati ya Pamoja (JTC) kutoka Tanzania Bw. Hamdouny Mansour (Kulia) na Kelvin Chibangula kutoka Zambia (Kushoto) wakisaini Hati ya Makubaliano ya Uimarishaji mpaka wa Kimataifa wa nchi zao mara baada ya kikao cha siku tano cha Kamati ya pamoja kilichofanyika katika mji wa Tunduma mkoa wa Songwe mwishoni mwa wiki.

Kiongozi wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania Bw. Hamdouny Mansour (Kulia) akipeana mkono na Bw. Kelvin Chibangula kutoka Zambia (Kushoto) mara baada ya kutia saini Hati ya Makubaliano ya Uimarishaji mpaka wa Kimataifa wa nchi zao wakati wa kikao cha siku tano cha Kamati ya pamoja kilichofanyika kwenye mji wa Tunduma mkoa wa Songwe mwishoni mwa wiki.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Na Munir Shemweta, WANMM TUNDUMA

Tanzania na Zambia zimetiliana saini ya makubaliano ya uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo.

 

Makubaliano hayo yamefikiwa mwishoni mwa wiki mara baada ya kukamilika kwa Kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu (JTC) kati ya Tanzania na Zambia kilichofanyia kwa siku tano katika mji wa Tunduma mkoa wa Songwe.

 

Utiaji saini makubaliano hayo umefanywa kati ya kiongozi wa timu ya Tanzania ambaye ni Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani  Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Hamdouny Mansour  na Bw. Kelvin Chibangula ambaye ni kiongozi wa timu ya wataalamu kutoka nchini Zambia.

 

Akizungunza mara baada ya utiaji saini makubaliano hayo, mkuu wa timu ya Tanzania Bw. Hamdouny Mansour amesema, katika siku tano za kikao hicho wataalamu wameweza  kupendekeza mawazo kwa utulivu, kuandaa bajeti pamoja na maazimio ya utekelezaji mpango wa uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo mbili.

 

"Niuhakikishie ujumbe wa wataalamu kutoka Zambia kuwa,Tanzania iko tayari kutekeleza yote yaliyopangwa kwa uwezo wa mwenyezi Mungu". amesema

 

Naye kiongozi wa timu ya wataalamu kutoka nchini Zambia ambaye ni Mpima Mkuu Msaidizi Bw. Kelvin Chibangula ameeleza kuwa, kikao hicho ni ishara ya ujirani mwema na ushirikiano imara wa kidiplomasia unaoendelea baina ya Tanzania na Zambia.

 

"Kikao hiki ni ishara ya ujirani mwema na ushirikiano thabiti wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Zambia" amesema

 

Wakati wa kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu (JTC), wajumbe walipata fursa ya kutembelea Mpaka wa Tanzania na Zambia unaoanzia alama Na. B588 (Mlima Nankugulu, wilaya ya Ileje) alama inayotengamisha Tanzania, Zambia na Malawi.

 

Mpaka wa kimataifa wa Tanzania na Zambia una urefu wa takriban km 345 ambapo km 100 ni nchi kavu, km 189 ni mto Kalambo na km 56 ziwa Tanganyika.

 

Lengo la kutembelea maeneo hayo ya mpaka ni kuwezesha kamati ya JTC Kuandaa bajeti na mpango kazi wa uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya Tanzania na Zambia.

 

Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya umoja wa Afrika kuwa ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za afrika iwe imeimarishwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.