Habari za Punde

Tume yataka wananchi kutazama Daftari la awali vituoni na kuhakiki taarifa zao




Wananchi wa Kata ya Kihesa katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mkoani Iringa wakikagua majina yao katika daftari la awali la wapiga Kura lililobandikwa katika kiuo cha kujiandikishia wapiga Kura kilichopo ofisi ya Mtendaji Kihesa. Tume Huru ya taifa ya Uchaguzi imeanza awamu ya pili ya Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura katika mikoa 15 ya Tanzania bara kuanzia Mei Mosi hadi 07, 2025 unaokwenda sambamba na uwekaji wazi wa daftari la awali. (Picha na INEC).


Na. Mwandishi wetu, Iringa

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imewataka wananchi kutoka katika mikoa 15 ya Tanzania Bara inayotekeleza mzunguko wa kwanza katika awamu ya pili ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura  na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kujitokeza katika vituo walivyojiandikishia na kutazama daftari la awali lilolowrekwa wazi na kutoa taarifa za wale waliokosa sifa kuwepo kwenye daftari hilo.

 

Akizungumza baada ya kutembelea vituo katika Halmashauri za Manispaa ya Iringa, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Halmashauri ya Mji wa Mafinga na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa, Mwenyekiti wa TumeHuru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele amesema wananchi wameonesha mwitikio katika siku ya kwanza ya zoezi hilo la siku saba na kuwataka kuhakiki taarifa zao.

 

Jaji Mwambegele amesema Tume imeweka wazi daftari la awali la wapiga kura katika vituo vyote vilivyotumika kuandikisha na kuboresha taarifa za Wapiga kura katika awamu ya kwanza, hivyo wananchi wajitokeze kuhakiki taarifa zao na kutoa taarifa za wale ambao hawastahili kuwepo katika Daftari hilo.

 

“Nawasihi wananchi endapo wataona katika Daftari ambalo tumeliweka katika kila kituo kuna mwananchi ambaye amekosa sifa kama vile kufariki basi wawe huru kwa kutumia fomu namba 5B kumuondoa huyo ambaye amekosa sifa za kuwepo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.”alisema.

 

Aidha, amesema yeye pamoja na viongozi wengine wa Tume wakiwepo Wajumbe wa Tume wametembelea mikoa yote inayotekeleza zoezi hilo na kushuhudia mwitikio wa watu vituoni, huku vituo vikifunguliwa kwa wakati uliopangwa wa saa 2:00 asubuhi.

 

“Wananchi wamejitokeza vizuri kuja kuboresha taarifa zao wale ambao hawakuboresha taarifa zao katika awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,”alisema Jaji Mwambegele.

 

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili unafanyika sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kuanzia Mei 01, 2025 na kukamilika tarehe 04 Julai, 2025.

 

Uboreshaji wa Daftari unafanyika kwa mizunguko mitatu ambapo mzunguko wa kwanza utajumuisha mikoa 15, mzunguko wa pili mikao 16 na mzunguko wa tatu utajumuisha vituo vya magereza na vyuo vya mafunzo.

 

Mikoa itakayohusika kwenye mzunguko wa kwanza wa uboreshaji ni pamoja na Iringa, Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia Mei 1 hadi 7 mwaka huu.

 

Aidha, mzunguko wa pili utahusisha mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia Mei 16 hadi 22, 2025.

 

Mzunguko wa tatu wa zoezi la uboreshaji wa Daftari utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye magereza ya Tanzania Bara na vituo 10 vilivyopo katika Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Juni 28 hadi Julai 04, 2025.

 

Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya pili, utafanyika ngazi ya kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya jimbo kwa Tanzania Zanzibar, ambapo jumla ya vituo 7,869 vitahusika, vituo 7,659 vipo Tanzania Bara na vituo 210 vipo Tanzania Zanzibar.

 

Katika awamu ya pili ya uboreshaji, wapiga kura wapya 1,396,609 wataandikishwa, wapiga kura 1,092,383 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 148,624 watafutwa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari,” amesema Jaji Mwambegele.

 

Mambo mengine ni kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa  taarifa za wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo.

 

Lengo la uwekaji wazi wa Daftari hilo ni kutoa fursa kwa wananchi kukagua, kufanya marekebisho ya taarifa za wapiga kura na uwekaji wa pingamizi dhidi ya wapiga kura waliomo kwenye daftari ambao hawana sifa na litabandikwa katika vituo vyote vilivyotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza.

 

Tume iliboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza kuanzia tarehe 20 Julai, 2024 na kukamilisha tarehe 25 Machi, 2025.

 

MWISHO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.