Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amefungua Kongamano la Nne la ZRCP

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na washiriki wa Kongamano la Nne kuhusu uwekezaji kwenye rasilimali watu kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde, Mtoni.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali itaendelea kujenga miundombinu ya kutosha ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.

Ameyasema hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika ufunguzi wa kongamano la nne kuhusu uwekezaji kwenye rasilimali watu, linalofanyika kwenye aukumbi wa Hoteli ya Verde, Mtoni.

Amesema serikali itazidi kujiekeza katika uwekezaji wa rasilimali watu ili kuchochea ubunifu wa teknolojia na kuimarisha utoaji huduma kwa umma na kuziwezesha biashara kuongeza faida na mitaji na kuwa na vijana wenye uthubutu na uwezo wa kubuni bidhaa mpya.

Amefahamisha kuwa kuna mabadiliko makubwa ya teknolojia duniani ambayo ikitumika vyema itasaidia kuwekeza kwenye watumishi wa umma ili watoe huduma bora na zenye gharama nafuu.

Aidha alisema la kongamano hilo ni kupata ufumbuzi wa vitendo na programu zinazoweza kuongeza ustadi wa watumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza ili kufanikisha azma hiyo, serikali imejidhatiti kuweka mazingira wezeshi katika uwekezaji wa rasilimali watu na ubunifu ili kuwavutia wawekezaji.

Mhe. Hemed amesema ushiriki wa taasisi zisizo za kiserekali, benki, kampuni za simu na nyenginezo ni muhimu hasa katika ukuaji wa rasilimali watu na ubunifu jambo linalodhihirisha dhamira na utayari wa kukuza rasilimali na ubunifu kwa ajili ya maendeleo.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Fedha na Mipango,   Naibu Waziri, Juma Makungu Juma amesema kongamano hilo ni muhimu katika kuijenga Zanzibar yenye maendeleo zaidi hasa katika sekta ya uwekezaji,

Makungu alisema kongamano hilo linaakisi dhamira ya serikali ya kuondoa pengo liliopo kati ya serikali na sekta binafsi na kufanya kazi pamoja ili kufikia maendeleo yatokanayo na ubunifu na uvumbuzi hasa wa kidijitali.

Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha vijana waliopo vyuoni na mitaani wanakuwa wavumbuzi na wabunifu wa teknojia ili kurahisisha kubadilisha mitazamo yao kuhusu kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa serikalini.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria Utumishi na Utawala  Bora, Mansura Mosi Kassim, amesema serikali inafanya mabadiliko katika sekta ya umma na kufanya mageuzi katika utoaji wa huduma kwa jamii kwa kutumia mfumo wa kidijitali ambapo baadhi ya taasisi za serikali zimeanza kutumia mifumo hiyo.

Ametoa wito kwa vijana kujikita zaidi katika matumizi ya teknolojia, ubunifu na uvumbuzi pamoja na kujifunza suluhisho la matumizi bora ya kidijitali

Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Utafiti, Uchambuzi wa Uchumi na Sera ya Jamii Zanzibar (ZRCP) Prof.  Mohammed Hafidh, aliishukuru serikali kwa kuendelea kuiunga mkono ZRCP jambo ambalo linaiwezesha kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Prof. Hafidh amefahamisha kuwa maelekezo na miongozo wanayopatiwa na serikali pamoja na viongozi yameifanya taasisi hio kupiga hatua na kusaidia katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

Alisema ZRCP inajipanga zaidi katika kuwapatia elimu vijana juu ya masuala mbali mbali yatakayowasaidia kufikia malengo waliyojiwekea.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)

Tarehe 27.08.2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.