Habari za Punde

Wakurugenzi wa Manispaa kushirikiana pamoja katika kuhakikisha wanalinda maadili na Utamaduni wa Mzanzibar .

Kamishna Idara ya Utamaduni Zanzibar. Dk Omar Salum Mohamed akizungumza katika kikao cha Mashauriano  na  Wakurugenzi wa Manispaa Unguja kuhusiana na ukiukwaji wa maadili katika Ukumbi wa Studio ya Filamu na Muziki ,Rahaleo.
Wakurugenzi wa Manispaa wakimsikiliza Kamishna Idara ya Utamaduni Zanzibar. Dk Omar Salum Mohamed (hayupo Pichani) katika kikao cha Mashauriano Huko Ukumbi wa Studio ya Filamu na Muziki ,Rahaleo.


Na Masha Juma .Idara ya Utamaduni. 05.08.2025.

Kamishna Idara ya Utamaduni Zanzibar. Dk Omar Salum Mohamed amewataka Wakurugenzi wa  Manispaa kushirikiana pamoja katika kuhakikisha wanalinda maadili na Utamaduni wa Mzanzibar .

Ameyasema hayo katika kikao Cha Mashauriano kati ya Idara ya Utamaduni na  Wakurugenzi wa Manispaa za Unguja  katika Ukumbi wa Studio ya Filamu na Muziki ,Rahaleo.

Amesema Baadhi ya Saluni za Kiume zimekuwa na utaratibu wa kuwaajiri wafanyakazi wa kike Kwa kuwahudumia wateja wa kiume na Saluni za wanawake kuhudumiwa na wanaume jambo ambalo ni kinyume na maadili ya Kizanzibar.

Aidha amesema   baadhi ya Wafanyabiashara hasa  wa mikahawa wanavaa nguo zinazoonyesha maumbile yao  jambo linapelekea ushawishi Kwa baadhi ya Wateja.

Amefahamisha kumejitokeza Mtindo kwa baadhi ya Madereva wa Bodaboda kukiuka masharti ya leseni Kwa kupakia  abiria wa Jinsia tofauti kwa pamoja .

Nae Mrajisi wa Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni ,Abdilahi Ramadhani Nyonje amesema wanashirikiana na Idara ya Utamaduni na Taasisi nyengine kutatua kero za Wananchi ikiwemo wanaopiga musiki Kwa sauti kubwa bila ya kuweka kithibiti  sauti (Sound Proof).

Hata hivyo amewaomba Wakurugenzi hao kushirikiana na Taasisi husika ili  kufikia malengo yaliopangwa na Serikali sambamba na  kulinda maadili ya Mzanzibar..

Kwa Upande wa  Wakurugenzi wa Manispaa  wamesema ni vyema kushirikiana kwa pamoja wakati wa kutoa leseni na kusimamia kanuni zilizopo ili kutoa adhabu kwa  wanaokwenda kinyume na Mila silka na Utamaduni wa Mzanzibar .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.