Mjumbe wa Bodi ya Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Said Sleiman Ali, amesema mafunzo ya sheria za uchaguzi kwa asasi za kiraia yatasaidia kuepusha changamoto zinazoweza kuwakumba wananchi.
Akizungumza katika ukumbi wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Mazizini, wakati wa mafunzo hayo, amesema hatua hiyo itawaongezea uwezo wadau hao katika kutoa elimu ya mpiga kura kwenye makundi mbalimbali ya jamii.
Ameongeza kuwa asasi za kiraia zitachangia pia kuimarisha ushirikiano na taasisi zinazohusika na sheria, jambo litakalosaidia kujadili changamoto na kutafuta ufumbuzi ili uchaguzi ufanyike kwa haki na salama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Wapiga Kura na Mawasiliano ya Umma wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Juma Sanif Sheha, amelishukuru Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu kwa kushirikiana na Tume hiyo katika kuzikumbusha asasi za kiraia sheria na kanuni za uchaguzi.
Amesema mafunzo hayo yamejikita katika kuwajengea uwezo waelewe maeneo muhimu ya kisheria, hususan kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba mwaka huu.
Nao Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumie, amesema wadau wa uchaguzi wakipewa mafunzo watakuwa chachu kubwa ya kuhakikisha uchaguzi unazingatia sheria na miongozo ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
Jumla ya asasi 60 za kiraia kutoka Unguja na Pemba zimeshiriki katika mafunzo hayo, sambamba na wadau wengine wakiwemo Jeshi la Polisi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar.
No comments:
Post a Comment