MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, akimuombea kura Mgombea wa Ubunge jimbo Makete Ndg. Festo Sanga katika Mkutano wa Ndani uliofanyika Katika Ukumbio wa CCM Wilayani Hupo.
Na MWANDISHI WETU, Makete
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uamuzi wa kumchagua Dk. Samia Suluhu Hassan awanie kiti cha urais kupitia CCM siyo kumpa zawadi bali ni kutokana na uwezo aliouonesha kuiongoza nchi kwa mafanikio makubwa.
Kimesema Dk. Samia licha ya kuichukua nchi katika mazingira magumu, lakini aliivusha salama na maendeleo makubwa yameshuhudiwa chini ya uongozi wake.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuendelea juwaunganisha Watanzania, kudumisha amani, umoja na mshikamano kwa miaka minne na nusu aliyoongoza akiwa mkuu wa nchi.
Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya mkoani Njombe, jana.
"Hatumpi zawadi, tunamwongeza muda wa kazi kwa sababu kazi yenyewe anaiweza, tunampa kazi anayoiweza, anayoijua. Kwa mfano umenunua gari jipya au ulikuwa nalo, lina dereva anaejua kazi yake uende uazime dereva wa muda halafu akiangusha tutapata wapi gari jingine, unampa dereva anayejua, mwenye leseni.
"Mamlaka haya ni leseni kwamba tulipewa leseni ya kuongoza Tanzania kwa miaka mitano tangu mwaka 2020, ikifika Oktoba 29, 2025 tutawaomba Watanzania 'kurenew' leseni yetu, sasa sifa moja ya "kurenew' leseni yetu ni kuwa na dereva mzuri, sasa kwa nini tuweke dereva mpya aje aangushe gari letu," alieleza.
Alisema Dk. Samia amefanya kazi yake vizuri kwa kipindi cha miaka mitano ndiyo maana mwaka huu watamchagua tena katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, kwa kuridhishwa na uongozi wake.
ALICHUKUA NCHI KATIKA
MAZINGIRA MAGUMU
Makamu Mwenyekiti Wasira alisema miaka minne iliyopita nchi ilikumbwa na maafa matatu, ambayo ni ugonjwa wa Uviko-19 ambao ulikuwa unaua watu na hauna dawa, ikaondokewa na Rais wa wakati huo (Dk. John Magufuli) ikiwa mara ya kwanza katika historia ya taifa kufiwa na rais akiwa kazini.
"Kufiwa na rais ambaye yuko madarakani katika nchi nyingine zenye shida ni sehemu ya mgogoro na unaweza kuingiza nchi ile vitani.
"Muone faida ya amani na faida ya umoja, alipofariki Mzee Magufuli nchi ikabaki imetulia... katiba ikatupa jibu kwamba akifa rais makamu wake ambaye waliomba naye kura ndiye anaapishwa kuwa rais. Makamu wetu alikuwa Samia Suluhu Hassan mwanamama, akatwambia maneno mawili 'Kazi Iendelee'
"Aliachiwa miradi mikubwa na marehemu, uchumi ulishuka kwa sababubya corona, ukaanguka kabisa na ukianguka uchumi maana yake umaskini unapanda.
"Mwanamama huyu tukampa nchi, tukamwachia utengenezaji bwawa la Nyerere lilikuwa asilimia 30, ajenge reli kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza mpaka Kigoma na kazi zingine za 'mabarabara' hata hii yenu ameimalizia yeye kwa sababu ilianzwa na Kikwete kipande, akaja Magufuli akafanya kipande lakini amekuja Samia akamalizia kwa hiyo ameweza," alisema.
Alisema kwa miaka minne amefanya mambo makubwa na kwamba hakuna mwenye shaka naye.
Kwa mujibu wa Sasira, Daktari Samia ameendesha nchi imeendelea kuwa moja, kuwa ya amani na maendeleo yamepatikana chini ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 ambayo wakati wa kuinadi alikuwa mgombea mwenza wa urais kisha yeye akawa mtekelezaji mkuu wake.
"Ninayo mifano michache ya hapa Makete kwenye elimu kwa mfano amejenga shule mbili mpya, lakini madarasa ya shule za msingi 143 mapya tena ya kisasa, sekondari amejenga nne mpya hapa Makete, amejenga madarasa 169 hapa Makete peke yake, hii siyo habari ya Tanzania ni habari ya Makete.
"Zahanati mpya amejenga tisa katika wilaya ya Makete yenye wapigakura 70,000, amejenga vituo vya afya vinne na ameimarisha hospitali iliyokuwepo.
"Umeme amesambaza asilimia 98 vijiji vyote vina umeme na vitongoji vinaanza kupata umeme na ilani yetu inasema ikifika mwaka 2030 kila mtanzania awe na umeme nyumbani kwake," alisema.
Aliongeza "Hakuna mwingine kama Samia labda atapatikana mwaka 2030 lakini kwa sasa ni Samia, kwa kipindi hiki Rais Samia amefanya kazi kubwa sana na ndiyo maana tunakuja kwenu kuwaambia 'Samia mitano tena'".
Wasira alitumia fursa hiyo kumwombea kura za Kishindo Dk. Samia, mgombea ubunge Jimbo la Makete Festo Sanga na wagombea udiwani waliosimamishwa na CCM katika jimbo hilo.
No comments:
Post a Comment