Makamu
wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza
na Balozi mteule wa Tanzania nchini Japan Mhe. Anderson Mutatembwa Ikulu
Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 16 Septemba 2025.
Makamu
wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika
picha ya pamoja na Balozi mteule wa Tanzania nchini Japan Mhe. Anderson
Mutatembwa mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma
leo tarehe 16 Septemba 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Balozi mteule wa Tanzania nchini Japan Mhe. Anderson Mutatembwa mara baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 16 Septemba 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi mteule wa Tanzania nchini Japan Mhe. Anderson Mutatembwa, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amemsihi Balozi Mutatembwa kuzingatia kipaumbele cha nchi ambacho ni diplomasia ya uchumi kwa kuhakikisha anavutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchini Japan pamoja na kuimarisha ushirikiano wa ubia.
Amemsisitiza Balozi Mutatembwa kuhakikisha makampuni ya Japan yanawekeza nchini Tanzania ili kuongeza thamani ya bidhaa hapa nchini na kuuza katika soko la Japan na soko la kimataifa.
Amesema ni vema kushawishi wamiliki wa viwanda kuwekeza nchini Tanzania hususani viwanda vya magari, viwanda vya dawa na vifaa tiba pamoja na viwanda vya bidhaa za kielektroniki.
Pia amesema kwa kuwa Japan inafanya vizuri katika sekta ya lojistiki ni vema kuvutia ushirikiano kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni lango kwa mataifa mbalimbali.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amemtaka Balozi Mutatembwa kuvutia uwekezaji katika sekta muhimu za kimkakati kama vile Utalii, Kilimo na Uvuvi pamoja na sekta ya Afya.
Amesema nchi ya Japan ni wabobezi katika matibabu ya magonjwa yasiyoambukizia kama vile magonjwa moyo na figo hivyo ni vema kuendelea kutafuta fursa za masomo ya ubobezi kwa Watanzania.
Pia ametaka kusimamia utekelezaji wa vipengele vya Mpango wa Ushirikiano kati ya Japan na nchi za Afrika pamoja na kusimamia hati za makubaliano na ushirikiano zilizopo baina ya miji ya Tanzania na Japan.
Makamu wa Rais amemsihi Balozi Mutatembwa kuwatambua na kuwaunganisha Watanzania wanaoishi nchini Japan ikiwemo kuwaonesha fursa ya kuchangia maendeleo ya Tanzania kwa kuwekeza nchini katika sekta ya makazi na biashara. Amemtaka kuwasisitiza mambo ya msingi ikiwemo kuzingatia sheria na taratibu za nchi hiyo ili kulinda heshima ya Tanzania.
Vilevile amemtaka Balozi Mutatembwa kuendeleza jitihada za matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Japan na kutafuta fursa zitokanazo na Kiswahili kama vile walimu na wakalimani.
Makamu wa Rais amempongeza Balozi Mutatembwa kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Japan. Amesema ni muhimu kuhakikisha anakuwa na nyenzo muhimu zitakazomuongoza katika uwakilishi nchini Japan ikiwemo Dira ya Taifa Maendeleo 2050, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na takwimu za msingi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Kwa upande wake Balozi mteule wa Tanzania nchini Japan Mhe. Anderson Mutatembwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuiwakilisha Taifa nchini Japan. Amesema atahakikisha analinda maslahi ya Tanzania na kuendelea kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu uliopo baina ya Tanzania na Japan.
Imetolewa na
Ofisi ya
Makamu wa Rais
16 Septemba
2025
Ikulu –
Chamwino.
No comments:
Post a Comment