Habari za Punde

JAMANI HATA KWENYE FOLENI BASI?

Si vizuri kuelezea au ndio utamaduni ambao visiwa vya Unguja na Pemba ni jambo la kawaida kwa watu kuwaona wengine si chochote si lolote au wengine hawana haki lakini wao wana haki kwa kuwa tu wana uhusiano fulani na jamaa mhusika au kuna wasta wa aina fulani ambao huutumia kwa wenyewe huona ni sawa lakini kwa wengi si uungwana.

Utamaduni huu hata mimi mwenyewe huko siku za nyuma nilikuwa nikiufanya kabla ya kusafiri na kuona jinsi nchi za wenzetu wanavyoheshimu taratibu na desturi walizojiwekea. Baadhi yetu wataweza kuniona mimi ndie kioja kwa kupoteza muda wangu na kuandika kuhusu jambo ambalo hata nifanye kitu gani basi ni kama kumpigia mbuzi gitaa.

Ninazungumzia tukio lililonikuta nikiwa katika foleni mojawapo hapo ZRB Kilimani mnara wa mbao nikisubiri kupatiwa leseni ya barabara – road licence.

Kioja cha kwanza ni kwamba tumekuwa hatuna tena utamaduni wa kuheshimu foleni. Walikuja jamaa wengine na kujiingiza katika foleni huku wakiona akina sisi wanyonge tupo pale kipindi tukipigwa na jua tukisubiri hilo wanaloliharakia wao kwa kuruka foleni. La kusikitisha zaidi hakuna hata mmoja anaejaribu kukemea halii hii isipokuwa kunun’gunika chini kwa chini ambako hakuleti athari yoyote.

Nilipojaribu kuzungumza na mmoja wa walio kwenye foleni alinijibu kwa masikitiko kwamba Visiwani hakuna tena anaemcha na kumuogopa Allah Subhaanahu Wata’ala. Na hii ndio moja ya athari zake.

Kioja cha pili kilichonisikitisha kushindwa kuvumilia pale walipokuja wengine ambao walitaka kuingia ndani ofisini ambapo nasi ndio tunapopataka na kuingia tu moja kwa moja bila ya hata kuonesha uungwana wa kuweza kutuomba tulio pale folenini au kwa uchache kutusalimia . Hutokomea ndani bila ya salamu au hata heshima ya kuonesha kwamba na sisi tuliopo paleni binaadamu kama wao na tuna haraka kama walizo nazo na tuna majukumu kama waliyo nayo wao.

Ama hiki cha tatu ni pale nilipomuona mmoja wa staff kama alivyoonekana akimuingiza sijui na jamaa au rafiki yake ndani kufanyiwa lile lile ambalo sisi tulioendelea kupigwa na jua tupo katika foleni bila ya hata kujali wala kuhisi au kujali tendo analolitenda. Ama kwa huyu sikumvumilia nilimwita kando na kumsalimu na kumuuliza suala dogo tu kwamba je kiendo alichokifanya anakiona ni sawa kumuingiza jamaa yake ndani na kudharau utaratibu uliowekwa na ofisi yake mwenyewe anayoitumikia. Alitaka kunipa maelezo mengi lakini nilimkatiza na kumuomba tu anijibu je ni sawa au si sawa?. Alinijbu tena kwa kujiamini kwamba ni sawa. Nilimwambia unaweza kwenda na jibu lako nimelisikia. na kutokana na jibu hili lililoniudhi katika nafsi yangu na nnaamini kwa mola wangu pia kwa kuona jinsi watu miongoni mwetu wanaodhulumu haki za wengine katika mambo ambayo wala mja hahitaji kufanya anayoyafanya isipokuwa ni kwa ujinga, jeuri, au ujahili wa kutofahamu nini maana ya kuheshimu utaratibu.

Baya zaidi ni pale wanaotoa huduma hizi wakiwaona watu hawa pia huwashughulikia kama ni kitu cha kawaida bila ya kujali au kuhisi kama wanatenda kosa kuwadhulumu wengine waliopo pale na mtu kuingizwa kinyemela. Kwa kuwa ni mfanyakazi mwenzao basi ana haki ya kupewa kipaumbele – preferential treatment.

Niliwahi kumuona meneja wangu kazini huko ughaibuni akijipanga foleni sawa na mimi mfanyakazi wa kawaida bila ya kujihisi wala kujiona kama yeye ana haki zaidi kwa kuwa ni meneja. Huu ndio uungwana. Huu ndio utamaduni wa kuukuza na kuuendeleza. Huu ndio mwenendo ambao ikiwa sisi tutausimamamia na kizazi chetu kitatuiga.

Tatizo linaloonekana ni wengi ambao ni walala hoi na wasio na uwezo wameikubali hali hii bila ya wao wenyewe kujaribu kuikemea.

Siwezi kuwabebesha lawama wasio na uwezo lakini pia sitoweza kuwaacha wanaovunja sheria hata zikiwa ndogo namna gani kwani tukianza na madogo kama haya ndipo jamii inaweza kurekebishika. Nimebahatika kuwepo nchi za wenzetu ambapo kila anaekuja na kukuta foleni huiheshimu na sijapatapo kuona mtu kukatiza au kujichomeka kwani wewe mwenyewe jinsi macho yatakavyokusuta na kukuandama utaona aibu.

Ama kwa wanaotumia uwezo wao kujiona kuwa wao ni wenye haki na wengine ni takataka tu waelewe kwamba kila atakaemdhulumu mwenzake katika dunia hata haki yake ndogo basi siku ya kiama Allah Subhaanahu Wata’ala atakuja kuilipa.

Unapokatiza kwenye foleni umewadhulumu wote walioko kwenye safu. Unapomuingiza jamaa yako kwenye safu au ofisini pia umedhulumu na ikiwa jamii itajengwa katika hali na mazingira kama haya basi tutegemee jamii isiyojua heshima wala kuheshimu haki za wengine na hatima yake ni kuwa na vurumai katika kila mambo yetu kwa kukosa mfumo unaoeleweka.

Basi jamani hata kwenye foleni hatuwezi kuwa na utaratibu utakaokubalika na wote kwa kuonekana wote tuna haki sawa?

Sidhani kwamba tunahitaji Malaika Jibriyl ‘Alayhis Salaam ashuke kutuongoza.
Mdau kutoka Ughaibuni

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.