Habari za Punde

KARUME BOYS YAPOKONYWA USHINDI DHIDI YA YEMEN

Timu ya soka ya vijana Zanzibar, Karume Boys imepokonywa ushindi dhidi ya Yemen katika mchezo wa fungua dimba baada ya kumchezesha mchezaji aliyezidi umri katika mashindano ya CECAFA chini ya umri wa miaka 20 inayoendelea Asmara Eritrea.

Karume Boys ilimchezesha Said Mussa Shaaban ambaye katika pasipoti yake amezaliwa April 1989 lakini kwenye kadi yake ya usajili ilionesha amezaliwa December 1993.

Katibu Mkuu wa CECAFA Nicholas Musonye alisema kwamba matokeo ya mchezo wa Yemen yamefutwa na badala yake ushindi wamepewa timu ya Yemen wa magoli 3-0. Pia kamati inaangalia uwezekano wa kuiadhibu zaidi kwani katibu mkuu alisisitiza; “ Tumepewa maagizo kutoka CAF na FIFA na tumetakiwa tuyadhibiti matokeo yote ya nidhamu pamoja uvunjwaji wa kanuni za michezo na hili ndilo nitakaloliangalia katika suala hili” Alisema.

“Hatujaweza kujifunza kutokana na matukio yaliyopita na hivyo kujiingiza katika udanganyifu ambao hauwezi kutupeleka popote” Alizidi kusisitiza.

Katibu Mkuu alisistiza kwamba pamoja adhabu waliyopewa Zanzibar bado suala atalipeleka mbele katika kamati za CAF na FIFA kwa adhabu zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.